Home Biashara UWEPO WA MATAPELI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA FEDHA

UWEPO WA MATAPELI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA FEDHA

0

Benki Kuu ya Tanzania imebaini uwepo wa Kampuni za kitapeli zinazodai kutoa mikopo kwa wananchi ndani ya muda mfupi baada ya kujiunga kwa kuweka amana kwa njia ya mtandao. Kampuni hizi ni pamoja na ile inayojiita VICOBA Foundation, ambayo imekuwa ikijinasibu kutoa mikopo ya kuanzia Shilingi za Kitanzania 2,000,000.00 hadi 10,000,000.00 baada ya mteja kulipia ada ya kujiunga ya kati ya Shilingi za Kitanzania 200,000.00 hadi 500,000.00. Aidha, ili kuvutia wananchi, Kampuni hii imekuwa ikiudanganya Umma kwamba ni Taasisi ya Serikali, jambo ambalo halina ukweli wowote. Aidha, uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba Kampuni hii haina hata ofisi ya kudumu. Vile vile, Kampuni hii imekuwa ikitumia majina ya viongozi wakuu wa nchi na watu mashuhuri katika kufanikisha utapeli wao yakiwemo majina ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hasan na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.

Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuufahamisha Umma kwamba mmiliki wa VICOBA Foundation kwa sasa anashikiliwa na Vyombo vya Dola ambavyo vinaendelea  na uchunguzi ili kuchukua hatua stahiki. Benki Kuu ya Tanzania kama Msimamizi wa Sekta ya Fedha, vikiwemo VICOBA, inapenda kuutahadharisha Umma kutojihusisha na huduma zozote zinazotolewa na Kampuni za namna hii  ili kuzuia upotevu wa fedha zao. 

Aidha, Benki Kuu ya Tanzania inatoa onyo kwa mtu, kikundi au taasisi yoyote inayojihusisha na biashara ya upokeaji amana na/au utoaji wa mikopo bila kuwa na leseni kuacha mara moja. 

Aidha, Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuukumbusha Umma kwamba Kifungu cha 6 (1) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, kinakataza mtu yeyote kufanya biashara ya benki au kupokea amana kutoka kwa Umma bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya 2018, kinakataza mtu binafsi, kampuni au kikundi kilichoanza biashara kuanzia tarehe 1 Novemba 2019 kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila kuwa na leseni halali inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania. Watu binafsi, makampuni na vikundi vilivyokuwa vinatoa huduma ya kupokea amana na/au kutoa mikopo kabla ya tarehe 1 Novemba 2019, vinapaswa kuomba leseni ya biashara kutoka Benki Kuu ya Tanzania kabla ya tarehe 31 Oktoba 2020 bila kukosa. 

Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu binafsi, kampuni au kikundi chochote kitakachofanya biashara ya kupokea amana na/au kutoa mikopo bila kuwa na leseni stahiki kwa mujibu wa Sheria.

Wananchi wanaombwa kutoa taarifa Benki Kuu ya Tanzania, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pale wanapopata taarifa za uwepo wa watu binafsi, makampuni au vikundi vinavyotoa huduma za fedha bila kuwa na leseni ya Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, wananchi wenye dukuduku au taarifa tajwa, wanahamasishwa kuwasiliana na Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania-Makao Makuu, Ghorofa ya 6 Mnara wa Kaskazini, S.L.P. 2939, Mtaa wa 2 Mirambo, 11884 Dar es Salaam au namba za simu +255-22-223-5483; +255-22-223-5584; au +255-22-223-5557 au barua pepe kwa [email protected]; [email protected]; na [email protected].

BENKI KUU YA TANZANIA

[email protected]  

9 Januari 2020