Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini
Bahuguna katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna akimkabidhi nakala ya Hati ya Utambulisho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) leo katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
******************************
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Shalini Bahuguna katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Waziri Kabudi amemweleza Bi. Shalini Bahuguna kuwa UNICEF imekuwa na mchango mkubwa sana kwa kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukuza, kulinda na kutimiza haki za watoto.
“Kwa ujumla UNICEF imekuwa ikisaidia Tanzania kufanikisha agenda zake za maendeleo endelevu ya kulinda, kukuza na kutunza haki za watoto…..na
tunaamini watoto hawa ni taifa la kesho”. Amesema Prof. Kabudi.
Waziri Kabudi amemueleza Bi. Bahuguna kuwa tangu mwaka 2016 Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na UNICEF, imefanikiwa kuboresha sekta za elimu na
afya ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa huduma bora za kijamii, kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na kuboresha huduma za maji katika mikoa mbalimbali ikiwemo, Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Kigoma, Njombe na Songwe.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) nchini, Bi. Bahuguna amesema kuwa UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea
kulinda haki za watoto.
“Haki za watoto katika taifa ni jambo muhimu sana, hivyo UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa pamoja na kupatiwa mahitaji muhimu”. Amesema Bi. Bahuguna.