Na.Alex Sonna
MBUNGE wa Singida Mashariki Mhe Miraji Mtaturu amegawa sare za shule,madaftari na kalamu zenye thamani ya shilingi milioni 6.8 kwa wanafunzi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza kwenye shule zilizopo jimboni kwake.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa katika mikutano yake ya kwanza jimboni humo baada ya kuchaguliwa na kuapishwa septemba 3 mwaka jana kuwa mbunge.
Akizungumza wakati akigawa vifaa hivyo Mhe Mtaturu amesema katika mikutano hiyo aliahidi kuwapatia wanafunzi 200 lakini kutokana na uhitaji wanafunzi hao wamefikia 350 na amewapatia wote.
“Serikali yetu ya awamu ya tano imewekeza kwenye elimu,inatoa elimu bila ya malipo,nami kama mbunge wa jmbo hili nimeona niunge mkono jitihada hizo kwa kusaidia sare na vifaa vya shule ili kusiwepo kikwazo na hivyo kuwezesha lengo la serikali kutimia,”alisema Mtaturu.
Amesema katika utendaji kazi wake kipaumbele chake cha kwanza ni elimu kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo.
“Enzi za uhai wake hayati Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kusema ukitaka kumsaidia maskini msomeshe mtoto wake,”alisema Mtaturu.
Amesema dhamira hiyo inaenda sambamba na kauli mbiu yake isemayo
“ElimuYetu,MaendeleoYetu”inayochochea upatikanaji wa elimu kwa wote ili iwe njia ya kupatikana kwa maendeleo.
Kwa upande wake afisa elimu wilaya Mwalimu Ngwano Ngwano akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri amempongeza na kumshukuru Mhe mbunge kwa dhamira yake ya kusaidia maendeleo wananchi kwenye sekta mbalimbali na kuwaomba wadau waendelee kuchangia sekta hiyo