Na. Majid Abdulkarim
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Gerald Mweli amewataka Makatibu Tawala wasaidizi wa Mikoa wa sehemu ya mipango, uratibu na usimamizi wa Serikali za mitaa nchini kuhakikisha kuwa mipango ya bajeti itakayoandaliwa katika mwaka 2020/2021 inakuwa na ushirikishwaji wa kutosha na umiliki wa viongozi katika ngazi zote nchini.
Mweli ameyasema hayo katika ufunguzi wa kikao kazi cha Makatibu Tawala wasaidizi wa Mikoa wa sehemu ya mipango, uratibu na usimamizi wa Serikali za mitaa nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano uliyopo katika ofisi za TAMISEMI jijini Dodoma.
Mweli amesema ushirikishwaji wa viongozi utaongeza mashirikiano katika uandaaji wa bajeti na kuboresha utendaji kazi ili kufikia malengo na kuandaa bajeti inayogusa mahitaji ya wananchi katika Mkoa husika.
“Uandaaji wa mipango na bajeti kipindi hiki umerahisishwa kwa kuwepo na mifumo ya Kieletroniki ya PlanRep kwa halmashauri na CBMS kwa Mikoa , hivyo hatuna sababu za kuwa na mipango na bajeti isiyokidhi viwango” Ameeleza Mweli.
Pia Mweli ameongezea kuwa Makatibu Tawala kuzingatia maelekezo ya viongozi wa kitaifa wafanyapo ziara katika maeneo yao ya kazi, vipaumbele vya Mkoa kulingana na fursa zilizopo na kuhakikisha maandalizi ya bajeti yanalenga kuimarisha utoaji wa huduma katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma na uendeshaji wa Serikali katika ngazi ya msingi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango OR-TAMISEMI John Cheyo amesema kila halmashauri inatakiwa kuwasilisha orodha ya miradi ya maendeleo kuanzia 2016 mpaka 2019 inayotekelezwa katika halmashauri zao.
“Naimani kubwa kikao hiki kitasaidia kuondoa changamoto mnazokutana nazo katika kuaanda bajeti katika maeneo yenu” ameongezea Bw.Cheyo.
Akitoa neno la utangulizi katika kikao hicho Mkurugenzi Tawala za Mikoa TAMISEMI Beatrice Kimoleta amesema ni kuwakumbusha Makatibu Tawala kufanya kazi zao kwa weledi unao takiwa ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi na kuwatumikia watanzania na taifa kwa ujumla ili kuleta maendeleo na kukuza uchumi.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya Mwajuma Nyamkomora akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wenzake amesema kikao hicho kimewapa mwanga katika kutekeleza majukumu yao na kimewaongezea uwezo kutaka kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya kazi.
“Natoa wito kwa TAMISEMI ni vyema utamaduni huu wa kutujengea uwezo kabla na baada ya kuaanda bajeti za mwaka husika zifanyike mara mbili kwa mwaka kabla na baada ya kuaanda bajeti ili kuwasilisha bajeti itakayoendana na matakwa ya mahitaji ya mikoa yetu” ameshauri Bi. Nyamkomora.