Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa(BMH) Dk.Alphonce Chandika, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu wagonjwa waliopandikizwa figo katika hospitali hiyo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya figo kutoka Japan, Prof.Kobayashi Shuzo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu wagonjwa waliopandikizwa figo.
Mkuu wa chuo cha Tiba cha UDOM Prof.Ipyana Mwampagatwa,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu wagonjwa waliopandikizwa figo katika hospitali ya Benjamin Mkapa.
Daktari bingwa wa magonjwa ya figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa(BMH) Dk.Kessy Shija,akitoa ufafanuzi kuhusu wagonjwa waliopandikizwa figo katika hospitali hiyo.
Mmoja wa wanufaika waliopandikizwa figo Bi. Leah Nkonoki,akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi alivyoweza kuokoa maisha yake kwa kupandikizwa figo.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa(BMH) Dk.Alphonce Chandika, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu wagonjwa waliopandikizwa figo.
PICHA ZOTE NA ALEX SONNA-FULLSHANGWEBLOG
………………………….
Na Alex Sonna,Dodoma
Hospitali ya Benjamin Mkapa(BMH), imefanikiwa kufanya upandikizaji figo kwa wagonjwa wengine wanne na hivyo kufikia 11 tangu kuanza kwa huduma hiyo.
Sambamba na hilo, upandikizaji huo umeweza kuokoa mamilioni ya fedha ambayo yangetumika kutibu wagonjwa nje ya nchi.
Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk.Alphonce Chandika, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wagonjwa waliopandikizwa figo.
Amesema awali kulikuwa na wagonjwa saba na Januari 6, mwaka huu wamewafanyia wagonjwa wanne ambao wote wanaendelea vyema pamoja na waliowapatia figo.
Ameeleza kutolewa kwa huduma hiyo kumeokoa fedha nyingi ambazo zilikuwa zikitumika kutibu wagonjwa hao nje ya nchi ikiwemo nchini India.
Amefafanua upandikizaji figo kwa mgonjwa mmoja kwenye hospitali hiyo unagharimu kati ya Sh.Milioni 22 hadi 25, na kwamba gharama ya matibabu hayo kwa nje ya nchi ni zaidi ya Sh.Milioni 100.
Dk.Chandika amesema gharama inayotumika kwa mgonjwa mmoja nje ya nchi inaweza kuhudumia wagonjwa watano katika hospitali hiyo na kwamba kwa wagonjwa saba wa awali ziliokolewa Sh.Milioni 700.
“Kwa wagonjwa ambao tumewafanyia huduma hii hakuna mgonjwa hata mmoja aliyepoteza maisha, wote wanaendelea vizuri,”amesema.
Aidha, amesema upandikizaji huo ulikuwa ukifanyika kwa kushirikiana na Chuo Kikuu ch Dodoma(UDOM) pamoja na wataalam kutoka Tokushukay Medical Corporation nchini Japan ambao baada ya upandikizaji huo wa watu wanne itakuwa ni mwisho kuja jopo kubwa kutokana na madaktari wa kitanzania kukomaa kwenye utoaji huduma hiyo.
Dk.Chandika amesema hospitali hiyo na wataalam wake wapo tayari kutoa huduma bora ya upandikizaji kutokana na ujuzi walioupata kutoka Japan.
“Tuna madaktari wanne ambao wamepata mafunzo kuhusu upandikizaji figo, hawa wameenda Japan mara mbili sio kwenda kuangalia bali kushiriki kabisa kwenye upasuaji na upandikizaji maana kule wenzetu wanafanya mara kwa mara,”amesema
Ameeleza kuwa wataalam hao wataitwa au kuombwa ushauri kama itatokea mmoja wa wagonjwa ana shida ambayo si ya kawaida.
Naye, Mwenyekiti wa jopo la wataalam kutoka Japan, Prof.Kobayashi Shuzo, amepongeza Tanzania kwa kuimarisha huduma za kibingwa ikiwemo za upandikizaji figo na kwamba hospitali hiyo mbali na kutoa huduma kwa watanzania wataweza kuhudumia pia wanaotoka mataifa mengine.
Kwa upande wake, Mmoja wa wanufaika wa huduma hiyo, Leah Nkonoki, amesema tangu amepandikizwa figo mwaka 2018 hajawahi kuumwa ugonjwa wowote na anaendelea na shughuli zake na alipewa figo na dada yake.