Mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake jijini Dodoma leo wakati akitoa taarifa ya kuokoa mamilioni ya fedha.
…………….
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dodoma imefanikisha kuokoa kiasi cha shilingi milioni mia moja hamsini na mbili laki tatu thelathini mia tatu themanini na mbili na senti ishirini na tano (152,330,382.25) baada ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ishirini na moja (21) yenye thamani ya shilingi bilioni sabini na sita milioni mia tatu ishirini mia tano arobaini na mbili na senti tisini na sita (76,320,268,542.96) inayofanyika mkoani Dodoma.
Fedha hizo zimeokolewa kwa kuwezesha kiasi cha shilingi milioni arobaini na mbili laki mbili tisini na nne mia tano themanini na mbili na senti ishirini na tano (42,294,582.25) zilizotumika kwa kazi nyingine kurejeshwa na kutumika kwenye mradi husika na kuuwezesha kuendelea, na shilingi milioni mia moja na kumi elfu thelathini na tano na mia nane (110,035,800/=) zilikatwa kama faini kwa mkandarasi kwa kuchelewesha kazi kukamilika ndani ya wakati.
Ufuatiliaji wa miradi hiyo katika sekta za elimu, afya, maji na ujenzi ulifanyika katika robo ya Oktoba hadi Disemba, 2019 ili kukagua iwapo thamani halisi ya fedha ilifikiwa ambapo ushauri na elimu ilitolewa katika maeneo ambayo yalikuwa na mapungufu yanayorekebishika. Aidha, miradi miwili ya ujenzi katika shule za sekondari yenye thamani ya shilingi milioni mia nne sabini na moja na laki sita (471,600,000/=) imeonekana kuwa na viashiria vya udanganyifu na rushwa katika matumizi ya fedha hivyo tunaichunguza iwapo kuna jinai.
Katika eneo la uelimishaji ili kuhamasisha jamii kushiriki kivitendo katika kukemea na kuzuia vitendo vya rushwa, TAKUKURU iliweka mkazo zaidi katika elimu dhidi ya vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, kampeni ya vunja ukimya: kataa rushwa ya ngono na kampeni ya UTATU inayopinga vitendo vya rushwa katika eneo la askari wa usalama barabarani, ambapo vipindi arobaini na tatu (43) vya redio na runinga vilirushwa, mikutano ya hadhara themanini na nne (84) na semina themanini na tisa (89) zilifanyika atumishi wa umma na ambapo washiriki ni wananchi na makundi ya wanasiasa, wanatumbi, sekta binafsi.
Pia katika kukazia makuzi ya maadili mema kwa vijana klabu mia moja na tatu (103) za wapinga rushwa katika shule za msingi, sekondari na vyuo zilifunguliwa na klabu mia ishirini na mbili (122) zilitembelewa na kuimarishwa.
Katika eneo la kupambana na rushwa, tulikamilisha uchunguzi wa majalada kumi na nne (14) na kufungua mahakamani kesi saba (7) zilizowahusu viongozi wa Ushirika wa akiba na kukopa, watumishi wa halmashauri na watu binafsi. Jumla ya malalamiko mia moja arobaini na saba (147) ya rushwa na makosa yahusianayo yalipokelewa ambapo maeneo yaliyoongoza ni Ardhi (asilimia 31.4); Serikali za mitaa (asilimia 22.9); Polisi (asilimia 14.3); Vyama vya siasa (asilimia 11.4); Mahakama (asilimia 4.3); Elimu (asilimia 4.3) na sekta zilizosalia asilimia 11.4. Ni muhimu wahusika wa sekta zinazolalamikiwa sana wajitafakari na kujirekebisha Kwa robo ya Januari hadi Machi, 2020, pamoja na majukumu mengine TAKUKURU itaendelea kuhamasisha jamii kuvunja ukimya na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa ya ambapo tunatarajia kuzishirikisha klabu za wapinga rushwa katika kutoa elimu hiyo.
Pia tutashirikiana na wadau wengine, likiwemo Jeshi la Polisi, kutangaza kampeni ya UTATU na kuhamasisha wananchi kutumia TAKUKURU App kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na jinai nyingine. Vile vile, kwakuwa huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu, tunaendelea kutoa elimu ya kujiepusha na kuzuia rushwa kwenye uchaguzi, kukusanya taarifa na kupambana kwa mujibu wa sheria na yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa inayohusiana na uchaguzi na nyingine.
Aidha, leo tunatarajia kuwafikisha mahakamani watu wanne kwa makosa mbalimbali ya rushwa. Wa kwanza ni Bw. James Gebu Kwangulija mwenye umri wa miaka ishirini na saba (27), mkazi wa Kikuyu Jijini Dodoma na ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa shahada ya kwanza ya ualimu wa masomo ya sanaa katika Chuo Kil kosa la kujaribu kutoa hongo ya shilingi laki tisa (900,000/=) kwa Afisa mitihani wa chuo hicho ili asaidie kuongeza ufaulu (GPA) za wanafunzi wenzake sita (6), kinyume na kifungu cha 15 (1)b cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa sura ya 329 marejeo ya 2018, Wa pili tutakayemfikisha mahakamani kwa makosa ishirini na sita (26) ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1)b cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa sura ya 329 ni Bw. Samwel Mosses Tuppah mwenye umri wa miaka thelathini na tisa (39), mkazi wa Tegeta Mivumoni, Kinondoni DSM ambaye ni Mchunguzi wa kuzuia maudhui yasiibiwe (Piracy Investigator) wa kampuni ya Multichoice Tanzania Limited (DSTV) ya Jijini DSM. Uchunguzi wetu umeonyesha kwamba kati ya mwaka 2017 hadi 2019, Bw. Tuppah aliomba na kupokea jumla ya shilingi milioni tano (5,000,000/=) kama hongo kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya Feisal Cable Networks ya Jijini Dodoma ili asichukue hatua kwa kampuni hiyo ya Dodoma kwa tuhuma ya kuiba maudhui ya DSTV.
Mwisho tutawafikisha mahakamani Bw. Rainer Alanus Kapinga mwenye umri wa miaka arobaini na tano (45) ambaye alikuwa Mganga Mkuu wa wilaya ya Bahi na Bw. Raymond Gaspary Mhegele mwenye umri wa miaka thelathini na tatu (33) ambaye ni Afisa TEHAMA wa halmashauri ya wilaya ya Bahi kwa makosa ya matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa sura ya 329, kughushi na kutoa nyaraka za uongo kinyume na Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 marejeo ya 2002. Uchunguzi wetu umeonyesha kwamba mwaka 2017 watuhumiwa walighushi na kuwasilisha kwa mwajiri wao stakabadhi za kiasi cha shilingi milioni tatu na laki tano (3,500,000/=) wakidai wamenunua vifaa vya TEHAMA huku wakifahamu kwamba ni uongo.
TAKUKURU inawaasa watu wote kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani mkono wa sheria ni mrefu. Tunawashukuru wananchi kwa kuendelea kutupa taarifa na tunazidi kuwasihi kuwa sehemu ya mapambano haya ili kuleta tija na kuboresha hali ya maisha ya watanzania wote.