Kati ya vyama hivyo, 2,532 sawa na asilimia 73.8 ni vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) ambavyo vilianzishwa wakati serikali ilipoanzisha Mfumo wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (JK Fund).
Akitoa rai hiyo jijini Dodoma Waziri wa Kilimo Mhe.Japhet Hasunga, amesema uamuzi huo utachukuliwa baada ya siku 90, tangu Mrajis wa Vyama Vya Ushirika kutoa tangazo kwenye gazeti la serikali.
“Vyama vingi ni matokeo ya mfumo wa uwezeshaji wananchi kiuchumi ujulikanao kama (JK Fund), ambao ulilenga kuwawezesha wananchi kiuchumi. Katika mpango huo wananchi walianzisha SACCOS kwa lengo la kupata mikopo kutoka kwenye mfuko huo,’ amesema.
Ameeleza sababu za kuchukua uamuzi huo ni vyama kutokuwa na ofisi tangu vilipoanzishwa, havijulikani vilipo wala viongozi wake, kutotayarisha taarifa za mapato na matumizi, kutofunga mahesabu na kufanyiwa ukaguzi pamoja na kutoitisha mkutano mkuu wa mwaka.
“Ninamuagiza mrajis wa vyama vya ushirika kutangaza kusudio la kuvifuta vyama 3,436 ambavyo havitekelezi majukumu yake ya msingi na havijulikani vilipo. Asilimia 78 ya vyama hivyo ni vya Akiba na Mikopo (SACCOS),” amesema Mhe.Hasunga
Mhe.Hasunga amesema vipo vyama vingine 1,250 vya ushirika vilivyosinzia huku vyama 6,463 ndivyo vilivyokuwa hai.
Mchanganuo wa vyama hivyo vinavyotarajiwa kufutwa ni SACCOS (2,537), vyama vya msingi vya wakulima- AMCOS (264), mifugo (82), walaji (25), huduma (72), ufugaji nyuki (17) na nyumba (8).
Vingine ni madini (23), viwanda (102), uvuvi (37), umwagiliaji (31), vyama vikuu (3) na vyama vinginevyo (235).
Ameitaja mikoa iliyoongoza kuwa na vyama hewa vya ushirika ni Mwanza (393) Pwani (335), Kagera (301), Morogoro (298), Arusha (282), Tabora (282) na Kigoma (207).
Kwa upande wake Naibu Mrajis wa Vyama Vya Ushirika nchini, Dk. Benson Ndiege, amesema hatua zinaendelea kuchukuliwa kwa viongozi waliotafuna mali za ushirika.
Katika hatua nyingine, Waziri Hasunga alitangaza kuwa Kamati ya Taifa ya Mbegu (NSC) imepitisha matumizi ya aina mpya 40 za mbegu bora zilizopendekezwa na Kamati ya Taifa ya Kupitisha Aina za Mbegu Mpya (NVRC).
Amesema kuwa mbegu hizo mpya aina 10 ni za mahindi, 2 za mpunga, 1 ya ulezi, 3 za pamba, 9 za muhogo, 9 za alizeti na mbegu sita za viazi vitamu.
Kwa mujibu wa waziri huyo amesema mbegu hizo mpya zitaanza kuzalishwa na kutumika nchini kuanzia msimu wa 2019/20, kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu.