Home Mchanganyiko TAASISI YA SPRF YAADHIMISHA MIAKA MITANO KWA MAFANIKIO, MTATURU AIPA UJASIRI

TAASISI YA SPRF YAADHIMISHA MIAKA MITANO KWA MAFANIKIO, MTATURU AIPA UJASIRI

0

 Viongozi mbalimbali wakifurahia maadhimisho ya miaka mitano ya Taasisi ya SPRF yenye makao yake makuu mkoani Singida.
 KatibuTawala wa Wilaya ya Singida, Wilson Shimo, akipata ‘champaign’ kwenye maadhimisho hayo.
  Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu akihutubia.
  Mkurugenzi Mtendaji wa SPRF, Dkt Suleiman Muttani akizungumza.
 Viongozi mbalimbali wakishiriki kukata keki kuashiria maadhimisho ya kimafanikio ya miaka 5 ya SPRF na Jamii. Kulia ni Padri Gilbert Mwilu, Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu na Mkurugenzi wa taasisi hiyo Dkt .Suleiman Muttani.
 Afisa ufuatiliaji wa SPRF, Mwedinuhu Beleko akizungumza kwenye hafla hiyo.
 Baadhi ya washiriki wakifuatilia tukio hilo.
 Watoto yatima na waishio kwenye mazingira magumu wakifurahia muda mfupi baada ya kupata chakula cha mchana na watendaji wa taasisi hiyo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa SPRF, Dkt Suleiman Muttani akikabidhi zawadi ya taulo za kijani kwa watoto njiti ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mandewa.


Mwonekano wa taulo za kijani kwa matumizi ya watoto wachanga zilizotolewa na SPRF kama zawadi kwenye maadhimisho ya miaka 5 ya taasisi hiyo.
Na Mwandishi Wetu, Singida
 
………………………………………………………………………….
TAASISI isiyo ya kiserikali ya Jiokoe na Umasikini yaani ‘Stars of Poverty Rescue Foundation’ (SPRF) hatimaye imetimiza miaka mitano ya utume na utumishi wake kwa jamii tangu kuanzishwa kwake huku Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu akiyataka mashirika mengine kuiga mfano wa juhudi za SPRF kama chachu ya mabadiliko dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa mwanamke na mtoto
SPRF ilianzishwa Desemba 2014 kwa malengo kadhaa, ikiwemo kuweka mazingira wezeshi katika kuchukua hatua za kuondoa umaskini wa kipato, kusaidia uimarishaji wa mifumo yenye kusaidia makundi ya watu walio katika mazingira magumu na hatarishi, na kuanzisha programu za elimu na afya ili kusaidia makundi athirika.
Malengo mengine ya taasisi hiyo, ambayo kwa sasa inafanya kazi zake chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS), ni kukuza ushirikiano miongoni mwa wadau na jamii, taasisi za kitaifa na kimataifa kwa lengo la kutokomeza umaskini wa kipato nchini na kwingineko, sambamba na kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika kukua na kutekeleza program endelevu.
Akitoa simulizi ya kusisimua ya sababu iliyowapa msukumo wa kuanzisha SPRF, wakati wa hafla ya kusherehekea tukio hilo, mkoani hapa jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk Suleiman C. Muttani, alianza kwa kusema umasikini una gharama kubwa!
“Ilikuwa kipindi cha majira ya kiangazi mwezi Julai mwaka 2014, wakati alipoitwa kumuona binti wa miaka 19 akiwa na tatizo linalojulikana kama uzazi pingamizi, na nilipomchunguza niligundua ana uambukizo mkali sehemu ya kondo la mtoto na kwenye via vya uzazi,”
Alisema binti huyo alikuwa hajaolewa akiishi na mama yake mzazi aliyekuwa mkulima mwenye kipato kidogo sana huko maeneo ya Merya..huku akiwa anajiuliza huenda binti huyo ametelekezwa na familia, lakini ukweli ni kwamba mama yake hakuwa na nauli ya kumpeleka hospitalini.
Muttani alieleza kwamba ukosefu wa fedha ukichagizwa na uelewa mdogo wa vidokezo vya hatari katika ujauzito, vilipelekea wazazi wamuite Mkunga wa jadi ili binti azalie tu nyumbani lakini mwisho wa siku pale nyumbani ilishindikana kujifungua.
“Hatimaye familia iliamua kumpeleka hospitali akiwa hoi, hajitambui. Alipofika hospitali tuligundua uzazi pingamizi na kumfanyia upasuaji ili kutoa mtoto na kuokoa maisha yake,” alisema Muttani.
Pamoja na juhudi zote zilizofanywa lakini siku ya tatu binti alipata fistula, akivuja mkojo hovyo bila kujitambua na alifariki dunia siku ya 9 akiwa hospitalini “Katika kujadili kifo hicho mimi na wataalam wenzangu wa afya tuligundua kwamba kifo hicho kingeweza kuzuilika ila alicheleweshwa kuja kwenye matibabu, uzazi pingamizi na uambukizi mkali ndizo sababu kuu za kifo chake,” alieleza
Alisema wao kama wataalamu hawakuwa na jibu la moja kwa moja la jinsi ya kukabili umaskini wa kipato cha familia yake, kama sababu kuu ya iliyopelekea binti huyo kupoteza maisha. Kifo hicho kinamaanisha kwamba “umaskini una gharama kubwa!…ya kwamba sadaka ya maskini ni kifo.
“Hivyo taasisi ya SPRF ilianzishwa kwa msukumo wa kifo hiki cha msichana kwa lengo la kusaidiana na serikali kutekeleza MKUKUTA kama suluhisho la gharama za umaskini, azma hasa ikiwa ni kujenga mazingira wezeshi katika kukabili umaskini wa kipato; na huo ndio ulikuwa mwanzo wa safari yetu,”
Kwa upande wake, Mtaturu akisisitiza juu ya madhara ya mila zilizopitwa na wakati, ukeketaji, na ukatili wa kijinsia hususan unaofanywa bila huruma kwa mwanamke na mtoto,…alisema vitendo hivyo bado vipo na ili kutokomeza inahitajika uwepo wa viongozi imara na jasiri hasa katika ngazi za vijiji.
“Naipongeza taasisi hii ya mfano ambayo siku zote imekuwa ikijielekeza kwenye baadhi ya malengo endelevu ya kitaifa na dunia kwa vitendo….mnatekeleza kikamilifu lengo namba moja la dunia ambalo linasema kusiwe na umaskini, lengo la tatu linahusu afya na ustawi na lengo la tano ni usawa wa kijinsia,” alisema Mtaturu.
Mbunge huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema sio jambo jepesi kuhamasisha masuala ya usawa wa kijinsia, haki za wanawake na watoto, na jamii kuachana kabisa na mila potofu, ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni ndani ya jamii ya watu wenye mitazamo na mapokeo tofauti tena ukiwataka kuacha mila zao wenyewe, na zaidi kuwafanya watu wenyewe wapinge mila zao.
Alisisitiza kwamba sio kazi ndogo kuwakusanya watu mahala pamoja na kuzungumza lugha yao, na hatimaye wao wenyewe kukubali, kubadilika na kugeuka kuwa kipaza sauti dhidi ya mila potofu na kandamizi…sio jambo jepesi hata kidogo!
“Kuna ustadi mkubwa katika mpangilio wa kazi zao na mawasiliano katika ngazi zote wanapotekeleza mradi, hufanya kazi zao bila kumwacha yoyote nyuma, nalisema hili kwa dhati kwa kuwa naifahamu vizuri taasisi hii tangu mwaka 2017 wakati nikiwa Mkuu wa Wilaya pale Ikungi,” alisema
Huku akionesha kufurahishwa na utendaji wa taasisi, Mtaturu alisema “Binafsi nimependezwa sana na mbinu zao za ushirikishaji viongozi wa serikali, wazee wa mila, viongozi wa dini na wazee mashuhuri katika kufikia malengo yao na zaidi kwenye uanzishwaji wa vikundi vya hamasa vya sauti ya mwanamke na sauti ya mwanafunzi kama mawakala wa mabadiliko kwenye kupinga ukatili wa kijinsia.”
Alisema pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Rais John Magufuli katika kuimarisha na kuitegemeza sekta ya afya katika kila nyanja nchini, bado vifo vitokanavyo na uzazi imekuwa ni tatizo huku akitoa rai kwa jamii kuungana na kuwa watekelezaji wakuu wa kupinga vitendo vyote vya ukatili na viashiria vinavyoweza kuzuia vifo hivyo nje ya sababu za kimatibabu
Mtaturu ambaye muda mwingi alitumia kupongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kitaifa, hususani suala linaloendelea la kasi ya usambazaji wa nishati ya umeme vijijini, alisema anaamini muda mfupi ujao jamii itabadilika kabisa na wimbo huo wa umaskini itakuwa historia.
Alisema mtu mwenye tashwishi ya utaifa na mwenye kujitoa ipasavyo katika kufanya kazi za kijamii ni lazima awe mtu mwenye kuguswa na changamoto; na falsafa zake zijengwe kwenye kuamini katika maslahi mapana ya utu, tunu na heshima.
Aidha, anapaswa kuwa mtu aliojiwekea nadhiri ya kuwa mtumishi wa jamii ajuaye tofauti ya umuhimu wa kutoa na kupokea, kuwa mwaminifu, anayeishi misingi ya ubinadamu na siku zote aliye tayari kujitoa, mbunifu na mwenye kujichunguza kama majivuno uliyonayo hayana nguvu kuliko hekima na unyenyekevu wako
Mtaturu aliwataka SPRF kutochoka wala kukata tamaa kutumikia jamii hata kama dhoruba ni kali, tofauti za kitamaduni zisiwatikise, huku akiwasihi siku zote kuendelea kuwa wavumilivu, wastahimilivu, wasiokimbia migogoro wala kujitengenezea migogoro na kukwepa kuendeshwa kwa matamanio ya utajiri na umaarufu usio na tija.
Alisema maadhimisho hayo yatukumbushe tulipotoka, tulipo na tuendapo. Tunaweza kuwa na historia na mitazamo tofauti lakini jambo la hakika kwa wote ni umoja wetu.
“Ni muhimu mno kujiuliza kwanini wewe uko hai na unafanya unayoyafanya sasa, mwisho wa siku hatutazamwi kwa yale tunayojifanyia sisi wenyewe bali pia kwa yale ambayo tulipaswa kuyafanya kwa wengine na hatukuyafanya,” alisema Mtaturu.
Awali Afisa Ufuatiaji wa SPRF, Mwedinuhu Beleko, alisema pamoja na mambo mengine taasisi hiyo kwa sasa inatekeleza mradi wa “AWARE,’’ kwa ufadhili wa FCS ambao azma yake ni utetezi wa haki kwa mwanamke na mtoto wa kike, kupinga mila potofu, masuala ya ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni, na ukatili kwa mtoto-huku idadi ya walengwa takribani 6000 kutoka kata 5 za Ikungi na vijiji 12 wamefikiwa.
Beleko alisema, ukeketaji hufanyika kwa siri sana kwa baadhi ya maeneo hasa nyakati za usiku, huku mtindo unaotumiwa kwa sasa ukiwageukia zaidi watoto wachanga hali inayohatarisha mustakabali mzima wa ukuaji wa mtoto kiafya, kimwili na kiakili.
Kuhusu mimba za utotoni Beleko alisema asilimia 7 ya wasichana nchini wanaolewa wakiwa na miaka 15, na asilimia 37 huolewa wakiwa na miaka 18. Wasichana wa umri huo bado hawajakomaa kukabili majukumu ya ndoa, uchungu na kujifungua.
Hata hivyo mradi huo wa ‘AWARE’ kwa mkoa wa Singida mpaka sasa umewafikia walengwa wa moja kwa moja 1875 kati yao 1336 walikuwa wanawake na 539 ni wanaume, wanajamii wengine wapatao 105,000 walifikiwa kwa njia ya vyombo vya habari.
“Sauti ya Mwanamke na Sauti ya Mwanafunzi ni vikundi tulivyovianzisha ndani ya maeneo ya utekelezaji wa mradi kama sehemu ya juhudi ya SPRF kushirikiana na jamii, lengo likiwa ni kuhamasisha na kuleta mabadiliko endelevu ndani ya jamii ile ile inayowazunguka kwa kuzingatia makundi rika, mathalani wanafunzi kwa wanafunzi wenzao kutoa ujumbe kupitia ngoma, mashairi, ngonjera, maigizo na midahalo,” alisema Beleko.
Maadhimisho ya miaka mitano ya SPRF yalikwenda sanjari na shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji wa zawadi za taulo za kijani za kuwafunika watoto waliozaliwa kabla ya muda “njiti” ndani ya Hospitali ya Rufaa Mandewa, kupata chakula cha mchana na watoto yatima na waishio katika mazingira hatarishi na kuwapatia vyeti na zawadi baadhi ya marafiki na wanufaika wa mradi.