Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma Grace Quintine wa pili kushoto mbele akiwa na baadhi ya wakuu wa Idara wa Halmashauri hiyo jana,
**********************************
Na Mwandishi Wetu,
Mbinga
WAKATI zoezi la undikishaji kwa ajili ya uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapiga kura likianza mkoani Ruvuma,baadhi ya wananchi wa Mji wa Mbinga,wameipongeza Serikali kupitia tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) kuanza zoezi hilo mapema kwa kile walichodai litatoa fursa kwa baadhi yao kushiriki katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana,wananchi hao Angelus Kapinga na John Kowelo wamesema, uamuzi wa uliofanywa na Tume hiyo kuanza mchakato wa uandikishaji na maboresho katika Daftari la kudumu la wapiga kura, ni ishara njema kwamba uchaguzi Mkuu ujao utakuwa huru na haki na Watanzania wengi watashiriki kuchagua viongozi wao kwa kuwa wengi watajiandikisha.
Angelus Kapinga alisema, yeye binafsi anafurahi kuona uchaguzi Mkuu wa mwaka huu atatumia haki yake ya msingi kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi kuanzia nafasi ya Udiwani,Ubunge na Rais kwa sababu katika uchaguzi wa Mwaka 2015 hakufanikiwa kupiga kura kwani alikuwa na umri chini ya miaka 18 ambao hauruhusiwi kisheria kupiga kura.
John Kowelo amepongeza uhamasishaji mkubwa unaofanywa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbinga mjini Grace Quintine, namna alivyojipanga kuhakikisha wananchi wenye sifa wanapata haki yao kujiandikisha katika Daftari la kudumu la Wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Mwezi Oktoba.
Alisema, Quintine ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mj Mbinga anapita kila mtaa na ma gari yenye vipaza sauti na wakati mwingine kwa miguu kuhamasisha kujitokeza katika vituo vya kujiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura, jambo linaloonekana kuwavutia watu wengi wa Mji wa Mbinga.
Kwa upande wake,msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbinga mjini Grace Quintine amewataka waandikishaji wasaidizi wa Daftari la kudumu la wapiga kura kuwa makini,kuzingatia sheria na kanuni za Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wote wa zoezi la Undikishaji wa wananchi katika Daftari la wapiga kura.
Amewataka waandishi hao, kuhakikisha wakati wote wanakuwa vituoni ili kuepuka usumbufu kwa wananchi wanaokwenda kujiandikisha.
Pia amewakumbusha kwenda kushirikiana na wadau wengine wakiwemo mawakala wa vyama vya siasa kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura katika maeneo yao.
Quintine ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mbinga,amewataka waandishi kutumia muda wa ziada kusoma kwa makini maelekezo yote waliyopewa wakati wa semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo ili kazi zao watekeleze kwa weledi.
Mbali na maagizo hayo,amewataka waandishi hao kutunza vifaa walivyopewa na Tume na kuhakikisha kila mtu mwenye sifa anayestahili kuandikishwa katika Daftari hilo anaandikishwa kama atakuwa na sifa.
Aidha, amewaonya kujiepusha kufanya kazi kwa miemko ya kisiasa na kwamba, Serikali inawaamini watatekeleza vema majukumu waliyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“mkafanye kazi zenu kwa kufuata na kuzingatia sheria na taratibu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi,shirikianeni na wadau wakiwemo mawakala wa vyama vya Siasa kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la kudumu la Wapiga kura,mjiepushe sana Itikadi za Vyama,mmekula kiapo kwa ajili ya kuwatumikia watu wote” alisema Quintine.