Mdau wa maendeleo wa Kata ya Magara Wilayani Babati Mkoani Manyara, Dkt Juma Muna akizungumza kwenye tamasha la Magara Salama 2019/2020 ambapo zaidi ya watu 2,000 walipatiwa elimu ya afya bila malipo.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria tamasha hilo la Magara Salama 2019/2020 lililofanyika kwa muda wa siku tisa.
*******************************
TAMASHA la Magara Salama 2019/2020 lililofanyika kwa muda wa siku tisa limekuwa na mafanikio baada ya wananchi 2,000 wa Kata ya Magara Wilayani Babati Mkoani Manyara, kupata elimu ya afya, wakiwemo 400 waliofanyiwa vipimo vya magonjwa mbalimbali bila kulipia.
Akizungumza kwenye tamasha hilo, mdau wa maendeleo wa kata ya Magara, Dkt Juma Muna ambaye kitaalamu ni daktari wa binadamu, alisema lengo la tukio hilo ni kuhakikisha elimu ya afya inawafikia jamii ya eneo hilo kwa urahisi zaidi kwani lilifanyika pia mwishoni mwa mwaka 2018.
Dkt Muna alisema zaidi ya watu 2,000 walipatiwa elimu ya afya na 400 walipimwa magonjwa bila malipo ikiwemo kisukari, malaria, ugonjwa ya moyo, shinikizo la damu, hali ya mlo, maambukizi ya virusi vya ukimwi, uzito na urefu.
“Hata hivyo baadhi ya wananchi hao walipimwa macho, wakiwemo watu wawili ambao watakwenda mjini Babati kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho,” alisema Dkt Muna.
Alisema pamoja na yeye kushiriki upimaji huo kutokana na taaluma yake pia shughuli hiyo ilifanywa kwa kushirikiana na wauguzi na madaktari wa kituo cha afya Magara.
Alisema aliandaa tamasha la Magara Salama 2019/2020 kwa lengo la kutoa elimu ya afya ya magonjwa tofauti kwa jamii na michezo mbalimbali ili kupambana na magonjwa yasiyoambukizwa na kuibua vipaji.
“Pamoja na mambo hayo mengi pia imetolewa elimu ya afya ya unyonyeshaji watoto kwa kina mama, uelewa wa wajawazito juu ya utunzaji wa mimba, chanjo kwa watoto na wanawake wengi wamenufaika nayo,” alisema Dkt Muna.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Magara, Mwanaidi Tatunga na Ruth Joshua wanaougua macho na kutakiwa kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa huo wamemshukuru Dkt Muna kwa hatua hiyo.
Joshua alisema hivi sasa gharama za matibabu ni kubwa hivyo wanapopata misaada kama hiyo wanapaswa kumshukuru Mungu kwani huduma na elimu imetolewa bila jamii kulipia.
Mariam Khalifa alishukuru huduma hiyo kutolewa bila malipo kwani wahitaji ni wengi na wasingeweza kugharamikia na wamefaidika na elimu ya afya iliyotolewa.
Tatu Mohamed alitoa wito kwa Dkt Muna kuwa na utaratibu wa kurudia huduma hiyo kwani watu wengi wanatamani kupatiwa huduma kama hizo ila wanakosa kipato kutokana na hali zao kuwa duni.