**********************************
02 Januari , 2020
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally amesema kuwa, CCM mwaka 2020 itaongoza siasa safi za uchaguzi, ni mwaka wa kudhihirisha CCM inaongoza siasa safi na kuheshimu maamuzi ya Umma kama ilivyofanya mwaka 2019.
Dkt. Bashiru ameeleza kuwa, CCM itakuwa mfano katika kuheshimu uamuzi wa umma katika uchaguzi, na CCM itashinda kwa kura nyingi kwa kuwa, zipo sababu nyingi za kuaminiwa na umma.
Dkt. Bashiru ameyasema hayo leo Januari 02, 2020 wakati akitoa salam za mwaka mpya 2020 katika mkutanao wa ndani wa wenyeviti wa mitaa na vijiji wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.
“CCM inatoa salam za mwaka mpya 2020, niwahakikishie wananchi wote wa Tanzania, mwaka huu tutaongoza siasa safi, na ni mwaka wa kudhihirisha CCM inaongoza siasa safi na kuheshimu maoni na uamuzi wa Umma, na itashinda kwa kishindo kwa kuwa wananchi walihitaji huduma ya maji sasa wanapata, walihitaji elimu bure sasa wanapata, walihitaji huduma za afya sasa wanapata na zingine nyingi, na siku zote wananchi sio wanafiki.”
Aidha ameongeza kuwa, Wapo watu wanalilia tume huru iwasaidie kupata ushindi, bila kufahamu kuwa, Tume huru haipigi kura bali inasimamia uchaguzi, kama chama hakina wapiga kura kisitegeme Tume iwape ushindi, CCM imewatafuta wapiga kura kwa kuwasomesha watoto bure, kutoa mikopo kwa wanafunzi, kujenga vituo vya afya, kusambaza maji, kujenga barabara, sasa wao waseme hao wapiga kura wamewapata kwa njia zipi kama ambavyo CCM inajipambanua.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu ameeleza msimamo wa CCM kuendelea kutetea haki za watu wote bila kujali jinsia, rika, dini wala kabila, ambapo akifafanua hilo amesema,
“CCM inapingana na udharirishaji ambao mara nyingi unajitokeza katika Uchaguzi Mkuu, wanawake kabla ya kugombea wanaitwa majembe lakini wakichukua fomu za kugombea wanaanza kuchimbwa na kuwekewa kashfa nyingi, wanajazwa hofu na wanaogopa, awamu hii CCM haitakubali wanawake wadharirshwe na haki ni lazima itendeke kwa wote.’’
Awali akimakaribisha Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera Bi. Costancia Buhiye amesisitiza zaidi umoja na mshikamo ndani Chama ambapo Katibu wa CCM wa Mkoa huo Ndg. Michael Chonya akisistiza umuhimu wa viongozi kusikiliza na kutatua kero za watu.
Katibu Mkuu yupo Bukoba mkoani Kagera kwa mapumziko ya siku kumi ambapo anatarajiwa kumaliza mapumziko hayo mwanzoni mwa mwezi Januari, 2020.