Na Mwandishi Wetu.
MABINGWA watetezi, Simba SC wameendelea kuwapa raha mashabiki wao baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya KMC jioni ya leo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
Ushindi huo wa tatu mfululizo chini ya kocha mpya, Mbelgiji Sven Ludwig Vandenbroeck unaifanya Simba SC ifikishe pointi 31 katika mchezo wa 12, ikiwazidi pointi saba sasa Kagera Sugar wanaofuatia nafasi ya pili ambao pia wamecheza mechi moja zaidi, wakati mahasimu wao wa jadi, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 21 za mechi 10.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Mbaraka Rashid aliyesaidiwa na washika vibendera Hamisi Chang’walu na Shaffi Mohammed wote wa Dar es Salaam Simba SC ilipata mabao yake yote kipindi cha pili na kwa mara nyingine tena wafungaji wote wageni.
Deogratius Kanda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliwanyanyua vitini mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kwa bao zuri dakika ya 46 akimalizia kazi nzuri ya kiungo mwenzake, Hassan Dilunga.
Na baada ya KMC kuwabana mabingwa hao watetezi sehemu kubwa ya kipindi cha pili, hatimaye kiungo Mbrazil Gerson Fraga ‘Viera’ akawafungia Simba SC bao la pili dakika ya 90 na ushei akimalizia pasi ya kiungo Mkenya, Francis Kahata.
Kikosi cha KMC kilikuwa; Jonathan Nahmana, Kelvin Kijiri, Ally Ramadhani, Abdallah Mfuko, small Gambo, Jean Baptiste Mugiraneza, Abdul Hilal/Rayman Mgungira dk87, Kenny Ally, Ramadhan Kapera, Hassan Kabunda/Rehani Kibingu dk71 na Bonphace Maganga/Serge Alen dk60.
Simba SC; Aishi Manula, Haruna Shamte, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Gerson Fraga ‘Viera’, Deo Kanda, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/Clotous Chama dk63 na Hassan Dilunga/Francis Kahata dk68.