Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina,akizungumza katika kikao cha wadau kujadili namna ya kunusuru Machinjio ya Dodoma kilichofanyika katika ofisi za Kampuni ya TMCL.
Kaimu Meneja wa machinjio ya Dodoma Victor Mwita,akijitambulisha katika kikao cha wadau kujadili namna ya kunusuru Machinjio ya Dodoma kilichofanyika katika ofisi za Kampuni ya TMCL.
Sehemu ya washiriki na waandishi wa habari wakifatilia hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhanga Mpina katika kikao cha wadau kujadili namna ya kunusuru Machinjio ya Dodoma kilichofanyika katika ofisi za Kampuni ya TMCL.
Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko Bw.Felix Nandonde,akizungumza katika kikao cha wadau kujadili namna ya kunusuru Machinjio ya Dodoma kilichofanyika katika ofisi za Kampuni ya TMCL.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina,akisisitiza jambo katika kikao cha wadau kujadili namna ya kunusuru Machinjio ya Dodoma kilichofanyika katika ofisi za Kampuni ya TMCL.
PICHA NA ALEX SONNA-FULLSHANGWEBLOG
……………
Na Alex Sonna,Dodoma
Serikali imevunja mkataba wa mauzo ya mali za machinjio ya Dodoma(TMCL) baina yake na kampuni ya NICOL uliosainiwa mwaka 2008 huku ikiitaka kampuni hiyo kulipa zaidi ya Sh.Bilioni 14.96 za madeni ya TMCL na mapunjo katika biashara ya machinjio kwa serikali.
Sambamba na hilo, Vyombo vya ulinzi na usalama vimeagizwa kuwachukulia hatua za kisheria watendaji wote wa NICOL, NARCO na TMCL waliohusika na ubadhirifu wa mali za TMCL na kuisababishia hasara serikali tangu mwaka 2008.
Hatua hiyo imefikiwa leo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina katika kikao cha wadau kujadili namna ya kunusuru machinjio hiyo.
Mpina amesema mkataba huo umevunjwa kwa kuzingatia Ibara ya 7 na 13 ya mkataba wa mauzo ya mali na hivyo kuanzia sasa machinjio hiyo itakuwa chini ya serikali.
“NICOL ilipe serikali Sh.9,712,127,660 ambazo serikali ilipunjwa katika biashara ya machinjio na pia NICOL ilipe madeni yote inayodaiwa kampuni ya ubia TMCL kiasi cha Sh.5,248,084,000,”amesema.
Aidha, ameitaka kampuni ya NARCO ijiondoe katika Kampuni ya Ubia TMCL ndani ya siku 60 kuanzia leo.
“Huduma za uchinjaji zitaendelea kutolewa kama kawaida katika kipindi cha mpito chini ya usimamizi wa serikali wakati mchakato wa kumpata mwekezaji mahiri wa mpito na wa kudumu unaendelea,”ameeleza.
Mpina amesema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk.John Magufuli ambayo imejipambanua kuwa serikali ya viwanda na wanyonge haitakubali hujuma na ufisadi uliokuwa ukifanyika katika machinjio hayo kuendelea.
“Aidha, nataka niwahakikishie kuwa waliohusika na wizi na ubadhirifu hawatapona, tunajua kuwa hata mishahara ya wafanyakazi nayo ilifanyiwa ufisadi na kuleta usumbufu mkubwa, pia tunatambua mahitaji ya uchinjaji mifugo na kusafirisha nyama nje ya nchi ambapo kusimama kwa machinjio hii kulisababisha wafugaji na vijana wengi kukosa ajira na masoko ya uhakika,”amesema.
Amewaomba wadau wote walioathirika kwa namna moja au nyingine na uendeshaji wa machinjio hiyo waipe muda serikali kushughulikia changamoto zilizopo.
“Katika kipindi cha muda mfupi machinjio ya Dodoma itafufuliwa na kupanuliwa na kuwa ya kisasa zaidi,”amesema.
Akizungumzia baadhi kasoro zilizobainika, Waziri Mpina amesema NICOL tangu ikabidhiwe mali hizo kwa kipindi cha miaka 11 haijawahi kutoa gawio kwa serikali.
Pia amesema nchi imepoteza ajira, fedha za kigeni, biashara na masoko ya mazao ya mifugo baada ya kiwanda kufungiwa kuuza mazao ya mifugo katika nchi za Jumuiya ya Kiarabu(UAE).
“Aidha, kampuni 10 zilisimama kusafirisha na kufanya biashara ya nyama baada ya kiwanda kufungiwa, ambapo kwa mwezi mauzo ya nyama nje ya nchi katika machinjio yalikuwa yamefikia tani 192 sawa na mbuzi 24,000 kwa mwezi, pia kiwango cha uchinjaji ng’ombe kushuka kutoka wastani wa ng’ombe 120 hadi 50 kwa siku,”amesema.