Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Chalamila, muda mfupi alipowasili kwaajili yakuongea naye na kumwelezea shabaha ya ziara hiyo mkoani humo.
Naibu Katibu Mkuu akizungumza na timu ya Afya ya Halmashauri ya Busokelo katika kituo cha Afya cha Isange kilichopatiwa Mil.500 nakufanikisha kujenga majengo 8 ambacho kinataraji kuanza kutoa huduma kuanzia mwezi Januari,2020.
Dkt. Dorothy Gwajima akitoa maelekezo katika Jengo la Hospitali ya Wilaya iliyopatia Bil. 1.5 ikiwa ni miongoni mwa Halmashauri 67 nchini zinazo jengewa Hospitali za Wilaya.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Busokelo Ramadhani Hussein, akijaribu kutoa utetezi wake mbele ya Naibu Katibu Mkuu hayupo pichani wakati wa ziara hiyo katika Hospitali Teule ya Itete.
Muonekano wa moja ya majengo ya Hospitali mpya ya Halmashauri ya Busokelo iliyopokea bilioni 1.5
Picha zote na Atley Kuni-TAMISEMI)
………………
Na. Atey Kuni, Busokelo-MBEYA
Serikali imetoa wiki mbili kwa timu ya Afya ya Halmashauri ya Busokelo mkoani Mbeya kutoa maelezo ya kina kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, kama ina uhalali wa kuendelea na majukumu yao yakusimamia Afya kwenye Halmashauri kutokana na uzembe mkubwa uliobainiwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Daktari Dorothy Gwajima wakati wa ziara yake ya kikazi.
Dkt Gwajima amefikia azma hiyo baada ya kutembelea Hospitali ya Halmashauri (Itete) na kusomewa taarifa ya afya ambayo, haijibu hoja za msingi ikiwemo usimamizi wa fedha, ushirikishwaji wa wajumbe wa timu ya usimamizi katika taarifa za mapato na matumizi ya fedha na utekelezaji wa mipango kwa ujumla.
Aidha, Dkt Gwajima alibaini hakuna taarifa za usimamizi wa vituo wala muhtasari wa vikao na michache iliyopo haijawahi kuthibitishwa wala haija fuata kalenda ya vikao kwa mujibu wa taratibu
“Hivi inakuwaje Mganga Mkuu wa Halmashauri huna muda na majukumu yako huelewi mambo ya msingi kifupi huna habari” alihoji Dkt Gwajima. “unao wajumbe wa timu ya afya idadi imekamilika, unao makatibu wa afya wawili, mnavyo vituo 22 tu vya kutolea huduma na vyote vinafikika, halafu hamjui chochote kinachoendelea, kwani mkiingia kazini huwa mnafanya nini hasa? Nako huko stoo ya dawa kumbukumbu haziko vizuri hii inakuwaje na kila siku tunaelimishana?”. Alizidi kuhoji huku akionesha kukerwa na mwenendo wa timu hiyo.
Kufuatia mambo kwenda ndivyo sivyo Naibu Katibu Mkuu alimuagiza Mkurugenzi kwamba ndani wiki mbili Mganga Mkuu Wilaya awe ametoa taarifa ya kina kwake lakini pia taarifa hiyo imfikie Katibu Tawala wa Mkoa pamoja na Katibu Mkuu TAMISEMI, ikitoa sababu za msingi kwa nini wasichulikuwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kutimiza wajibu wao.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Busokelo Eston Ngilingwa, amekiri ziara hiyo ya Naibu Katibu Mkuu kumfumbua Macho na kuanzia sasa atatumia mbinu na mikakati hiyo na kufanya suala la dawa kuwa ajenda mtambuka na ya kudumu kwa viongozi wote wa Halmashauri hiyo wanapokutana lakini pia Mkoa.
“Ndugu Naibu Katibu Mkuu kwa kweli mimi umenipa somo jipya ambalo hata kuongea nashindwa niongee nini maana kila ulichokiona hapa hakuna mtu ambaye anaweza kusema amesingiziwa, hivyo naomba kuahidi kufanyia kazi maelekezo yako na nitatoa taarifa mimi mwenyewe” alisema Ngilingwa.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dkt. Ramadhani Hussein, mbela ya Naibu Katibu Mkuu, alikiri kushindwa kusimamia eneo lake la kazi huku akiomba msamaha kwa kushindwa kufanya hivyo na kuahidi kubadili katika utendaji wake.
Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, anayeshughulia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima, amekuwa na muendelezo wa Ziara zake kwenye Mikoa mbalimbali nchini kujionea uendeshaji wa shughuli za Afya kwa Ngazi ya Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati, ambapo kote anakopita amekuwa akisisitiza watumishi wa kubadilika kifikra na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani katika awamu ya sasa ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye ameamua Taifa lifikie uchumi wa kati ifikapo 2025, lazima suala la Afya liwe kipaumbele namba moja kwa wananchi.