Na.Alex Sonna,Dodoma
JESHI la Polisi mkoani Dodoma limetolea ufafanuzi kifo cha Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiislamu ya Dalai na mmiliki wa Shule ya Zamzam, Ustaadhi Rashid Ally Bura kilichotokea Desemba 22 mwaka huu.
Tangu kutokea kwa kifo hicho kumekuepo na taarifa nyingi zinazosambazwa zikieleza kuwa mwili wa Ustaadhi Bura ulikutwa ukiwa na majeraha jambo ambalo Polisi wamelikanusha.
Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP Gilles Muroto amesema baada ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na madaktari kuufanyia uchunguzi mwili ww Ustaadhi Bura iligundulika amefariki baada ya kupata na tatizo la moyo.
” Napenda kutoa ufafanuzi wa kifo cha Ustaadhi Bura ambaye ni mmiliki wa Shule ya Zamzam kuwa mauti yalimkuta baada ya kupatwa na tatizo la moyo na kukosa msaada wa haraka.
Sasa kumekuepo na taarifa kutoka sehemu mbalimbali zikisema kwamba Ustaadhi Bura mwili wake ulikua umeshambuliwa wengine wakisema alikatwa sehemu zake za siri jambo ambalo ni uzushi na ukweli wa kifo chake ni huu ambao tunausema sisi,” Amesema SACP Muroto.
Amesema mwili wa Marehemu ulikutwa ofisini kwake ukiwa tayari umepatwa na umauti na ulikua umeharibika kwa kuvimba na kutoa harufu baada ya kukaa kwa siku nne.
Kamanda Muroto amesema baada ya Jeshi la Polisi kufika ofisini kwake walifanya uchunguzi na upekuzi katika ofisi yake na kugundua hakukua na uharibifu wowote wala wizi uliofanyika.
Wakati huo huo Kamanda Muroto amewataka wananchi mkoani Dodoma kusherehekea kwa amani sikukuu ya Mwaka mpya bila kufanya vurugu na kwamba Jeshi la Polisi halitomvumilia mtu yoyote ambaye atajaribu kuvunja amani.
” Niwapongeze wananachi wetu kwa kusherehekea Krisimasi vizuri niwaase pia katika sikukuu ya Mwaka washerehekee kwa utulivu na amani bila kufanya vurugu zozote ambazo zinaweza kuhatarisha amani ya Mkoa wetu, ” Amesema Kamanda Muroto.