Watalii zaidi ya 450 kutoka Israel wamewasili nchini mwezi Desemba 2019 kwa ajili ya tembelea vivutio vya kitalii vilivyoko kaskazini mwa Tanzania. Watalii hao wamekuja nchini kwa kutumia ndege binafsi na za kawaida.
Kundi la kwanza la watalii 150 liliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) tarehe 21 Desemba 2019 na kupokelewa na Bodi ya Utalii nchini (TTB) na baadaye kuelekea katika vivutio vya utalii vilivyoko mkoani Arusha.
Kundi la pili na la tatu lililokuwa na watalii 305 limewasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege KIA tarehe 24 Desemba 2019.
Watalii hao wako nchini kwa ajili ya kusherehekea sikukuu za Krismass na Mwaka mpya wanatembelea Hifadhi za Taifa za Serengeti, Tarangire, Ziwa Manyara, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro na Bonde la Eyasi.
Ubalozi wa Tanzania nchini Israel umetoa viza zaidi ya 500 kwa Waisrael ambao wamepanga kuwasili nchini kwa kutumia Mashirika ya Ndege ya Ethiopia, Uturuki na Uswisi katika kipindi hiki cha siku kuu za mwisho wa mwaka huku ukiendelea kuratibu ziara nyingine ya watalii zaidi ya 800 ambao mchakato wa safari yao upo katika hatua za mwisho.
Ujio wa watalii hao unatokana na jitihada za kuvutia watalii zinazofanywa na Ofisi ya Ubalozi nchini Israel kwa kushirikiana na makampuni ya wakala wa utalii ya ndani na nje ya nchi ili kuunga mkono harakati za Serikali za kukuza pato la taifa kupitia utalii na hivyo kuiletea nchi maendeleo.