Mabingwa wa kihistori Tanzania bara Yanga wameshindwa kutamba katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya mara baada ya kutoka sare ya bila kufungana na wenyeji Mbeya City.
Sare hiyo imeipunguzia kasi Yanga ambayo ilikuwa inawafukuzia wapinzani wao Simba taratibu ambao kwa sasa wamewaacha kwa jumla ya pointi saba wakiwa ila Yanga ina mchezo mmoja mkononi.
Yanga imecheza jumla ya mechi 8 na ina pointi 18 huku Simba ikiwa imecheza mechi 10 na ina pointi zake 25 kwa sasa.
Mchezo ulikuwa na ushindani kwa timu zote mbili huku kila timu ikitengeneza nafasi kwa kushtukiza na kushindwa kuzitumia kutokana na umakini wa mabeki wa timu zote mbili.
Yanga ilianza kufanya mabadiliko kipindi cha pili ambapo ilimtoa Said Juma dakika ya 61 na nafasi yake ikachukuliwa na Mrisho Ngassa ambaye alifanya majaribio mawili ambayo hayakuazaa matunda.
Kwa upande wa Mbeya City wao walifanya mabadiliko dakika ya 67 kwa kumtoa Majaliwa Shaban na nafasi yake ikachukuliwa na Seleman Shaban na dakika ya 79 alitoka Idd Gammba na nafasi yake ikachukuliwa na Kelvin John kabla ya Notikasa Masasi kutoka dakika ya 85 nafasi yake ikahukuliwa na Seleman Mangoma na mabadiliko hayo hayakuleta matunda.
Kadi mbili za njano zimetolewa kwenye mchezo wa leo ambapo zote zimekwenda kwa Yanga kupitia kwa Deus Kaseke na Jaffary Mohamed .
Ligi hiyo inatarajia kuendelea kesho bingwa mtetezi Simba atakuwa uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kumenyana na Lipuli FC kutoka mkoani Iringa.