Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akiwahutubia viongozi na wafanyakazi wa Wilaya ya Nzega hivi karibuni wakati wa mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya siku tatu ya kuhamasisha kilimo ikiwemo pamba na upandaji wa miti.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akiwahutubia viongozi na wafanyakazi wa Wilaya ya Uyui hivi karibuni wakati wa mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya siku nne ya kuhamasisha kilimo ikiwemo pamba na upandaji wa miti.
Mkuu wa Wilaya ya Uyui Gift Msuya akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kuwahutubia viongozi na wafanyakazi wa Wilaya ya Uyui hivi karibuni wakati wa mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya siku nne ya kuhamasisha kilimo ikiwemo pamba na upandaji wa miti.
********************************************
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani Nzega kumsaka na kumkata Karani wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Ikwabansabo kwa tuhuma za kutoroka na shilingi milioni 15.9 za wakulima wa pamba.
Alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni Raphael Malimbi alikiuka taratibu za uchukuaji wa fedha kwa ajili ya malipo ya mauzo ya pamba ya wakulima ambapo alichukua fedha taslimu badala ya kuwalipa kupitia akaunti za wakulima za Benki au simu za mkononi.
Mwanri alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wa majumuisho na watendaji wa vijiji , kata , Maafisa ugani na Watumishi wa Wilaya ya Nzega ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu kuhamasisha kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo pamba.
Alimtaka Kamanda wa Polisi Wilaya(OCD) ya Nzega SSP Constatine Mbogambi kuhakikisha ndani ya saa 24 mtuhumiwa anamkamatwa na kuanza taratibu za kumchululia hatua za kisheria ikiwemo kumfikisha Mahakamani.
Mwanri alisema hatua ya kwanza ya kufanikisha hilo ni vema Jeshi la Polisi likaanza kwanza kumkata Diwani wa Kata ya Milambo Itobo ambaye ndiye aliyedhamini mtuhumiwa na kudai kuwa atalipa pesa hiyo ya wakulima.
Alisema Serikali haiwezi kukubali vitendo vya kuwadhulumu wakulima fedha zao vikaanza upya kwani ndivyo vilivyosababisha wakachukia ushirika katika miaka ya nyuma.
Mwanri aliwaonya viongozi wengine ambayo wamechaguliwa kusimamia vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) kutodiriki kugeuza Ushirika ni sehemu ya kujipatia fedha kinyume cha sheria.
Alisema kama kuna kiongozi amejiingiza katika uongozi wa AMCOS ili kupata utajiri amekosea njia ni vema akaondoka mapema kabla ya hatua mbalimbali dhidi yake hazichukuliwa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa aliwaonya Maafisa Ushirika wa Halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha wanajiridhisha uhalali wa malipo kabla ya kuyapitisha.
Alisema ikibainika kuwa Afisa Ushirika yoyote alishiriki katika malipo machafu atachukuliwa hatua ikiwemo kufukuzwa kazi.
Aidha Mwanri alisema kama kuna wakulima wa Pamba ambao bado wanadai ni vema Maafisa Ushirika hao wakaorodhesha majina ya wakulima ambao bado wanadai na kuyapeleka kwa Wakuu wa Wilaya kwa ajili ya kufuatilia malipo ya wakulima.