Wafanyakazi wa TTCL Corporation wakiwa katika zoezi la kuchangia damu kwenye kituo cha damu cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) leo jijini Dar es Salaam. |
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation), Bw. Waziri Kindamba akichangia damu katika kituo cha damu cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) leo jijini Dar es Salaam. |
Na Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Bw. Waziri Kindamba leo wamejitokeza kuchangia damu katika kituo cha damu cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Akizungumza katika zoezi hilo Mkurugenzi Mkuu, Kindamba alisema TTCL kwa mwaka huu imeona isherehekee kwa namna tofauti kwa Shirika kupitia Wafanyakazi wake kutoa zawadi ya kuchangia damu, tukio linaloonesha upendo wa kipekee katika kuokoa maisha ya ndugu, jamaa na Watanzania wote waitaji.
Alisema msimu wa Krismasi ni wakati wa kuonesha upendo, kushukuru kwa mambo mengi ambayo yamepita katika mwaka mzima. Kindamba alibainisha kuwa TTCL inaamini kuwa damu waliochangia itaenda kuziba pengo la uhitaji katika benki ya damu MNH, na pia kuokoa maisha ya baadhi ya Watanzania.
“Ni vyema tukatambua kuwa kuchangia damu si tu kwamba ni suala la kibinadamu katika kusaidia watu, bali pia ni thawabu kubwa kwa Mwenyenzi Mungu. Tafiti mbalimbali zinaonesha watu walio katika uhitaji wa damu ni pamoja na Mama Wajawazito, Watoto, Wagonjwa wa upasuaji na wahanga wa ajali za moto na barabarani. Hivyo tumetambua hili na kuzingatia kuwa yawezekana tukawa wahanga siku moja na kuhitaji huduma ya damu,” alisema Kindamba.
Aidha aliongeza kuwa TTCL Corporation inachukulia tukio hilo kama sehemu ya huduma kwa jamii, ambayo Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Corporation linajisikia fahari kuitoa na kuihudumia jamii, hivyo kutoa rai kwa Watanzania wote kujitokeza kuunga mkono juhudi za kuchangia damu.
“Nipende kutumia nafasi hii kuihamasisha jamii na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kuweka utaratibu wa kuchangia damu kwani janga kubwa la kibinadamu kwa sasa ni upungufu mkubwa wa upatikanaji wa damu salama na kwa wakati muafaka,” alisisitiza Mkurugenzi Kindamba.
Kwa upande wake, Afisa Muhamasishaji Damu Muhimbili, John Daniel Bigambalaye amewapongeza wafanyakazi wa TTCL kujitokeza kuchangia damu kwa hiyari hivyo kuwaomba mashirika mengine na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kuchangia damu.
Baadhi ya Wafanyakazi wa TTCL Corporation wakichangia damu kwenye kituo cha damu cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) leo jijini Dar es Salaam. |
Alisema uhitaji wa damu Hospitali ya Taifa Muhimbili ni mkubwa na damu haitengenezwi popote zaidi ya kuomba kwa raia wenye afya njema kujitokeza na kuchangia damu. Alisema takribani chupa 200 za damu hutumika kwa siku katika hospitali hiyo kuokoa maisha ya wahitaji hivyo kuomba Watanzania kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wahitaji.
“Ni jukumu letu sote kubeba dhamana ya kuokoa maisha ya wenzetu na ya kwetu wenyewe kwakuwa mstari wa mbele kuchangia damu ili kuhakikisha watu wa rika zote wanapata fursa ya damu kwa gharama nafuu na kwa wakati,” alisema Bigambalaye.