Serikali imeeleza kuwa imekusudia kuanzisha juhudi wezeshi kuhakikisha kuwa mbegu bora za kilimo zinazalishwa nchini ili kuondokana na wimbi la uagizaji wa mbegu nje ya nchi.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 22 Disemba 2019 mara baada ya kutembelea kampuni ya Namburi inayojihusisha na uzalishaji wa mbegu za vizazi za mahindi, mtama na mpunga iliyopo katika eneo la Vwawa wilayani Mbozi wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Songwe.
Amesema kuwa Tanzania ina uhitaji wa mbegu kiasi cha Tani 186,000 za mazao mbalimbali huku uzalishaji wa ndani ikiwa ni pamoja na uagizaji wa mbegu nje ya nchi ukiwa bado mdogo kwani haujafika hata Tani 50,000.
Amesema kuwa Tanzania ina maeneo makubwa na bora kwa uzalishaji hivyo ni lazima kuzalisha mbegu za kutosha nchini na kuachana na utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi.
Waziri Hasunga ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha kuwa wananunua mbegu bora kwa ajili ya kukabiliana na msimu wa kilimo na kuachana na matumizi ya mazao yao ya misimu iliyopita waliyoyahifadhi kama mbegu.
Katika ziara hiyo waziri Hasunga amezungumza na wananchi wa kijiji cha Mbulu kilichopo katika kata ya Mahenje wilayani Mbozi mara baada ya kukagua skimu ya umwagiliaji ya Mbulu amesema kuwa serikali imedhamiria kuimarisha skimu za umwagiliaji nchini ili kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua.
Mhe Hasunga amesema kuwa kilimo cha kutegemea mvua ni hatari kwani hakina uhakika wa upatikanaji wa chakula cha kutosha kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza za kukosekana kwa mvua kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi.
Amewaagiza maafisa ugani kuzuru katika maeneo ya wakulima ili kutoa elimu sahihi za kilimo, matumizi sahihi ya viuatilifu pamoja na matumizi sahihi ya zana za kilimo.
Ameitaja Programu ya kuendeleza kilimo awamu ya pili-ASDP II yenye jukumu la kuimarisha masoko na kuongeza thamani kuwa ni lazima wakulima watumia njia bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kupata elimu bora na sahihi kwa wakulima.
Waziri Hasunga amesema kuwa katika Programu hiyo ya kuendeleza kilimo awamu ya pili moja ya mambo msingi ni matumizi bora ya maji na ardhi, hivyo sekta ya kilimo ni muhimili wa matumizi bora ya maji kupitia skimu za umwagiliaji.