Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu waliokutana kujadili namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu kilichofanyika jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt.Francis Michael akitoa mada kwa Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu kilichohusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu kilichofanyika jijini Dodoma.
Mkuu wa Uelimishaji kutoka Taasisi ya Kupambana na Kutokomeza Rushwa TAKUKURU Bw. Asseri Mandari akitoa mada kuhusu jitihada za Taasisi hiyo katika kupambana na rushwa ya ngono katika sehemu za kazi na katika Sekta ya elimu hasa elimu ya juu katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma kilichohusu namna ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu.
Baadhi ya Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma kilichohusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika Taasisi na Vyuo vya elimu ya juu nchini.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
…………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAKATI vitendo vya ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono vikidaiwa kushamiri katika Vyuo vya elimu ya juu hapa nchini, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii imeibuka na kutangaza mkakati wa kutokomeza tatizo hilo.
Hayo yamebainishwa leo jijini hapa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. John Jingu, wakati akifungua kikao kilichowakutanisha wawakilishi wa vyuo vya elimu ya juu kilichoketi kwa lengo la kuzungumzia namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika maeneo ya Vyuo vya elimu ya juu.
Dkt. Jingu amesema kuwa katika kuhakikisha vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono vinakomeshwa hapa nchini, Serikali na Wadau wengine watajikita katika kutekeleza mkakati wa kukomesha kwa asimilia 50 hadi ifikapo 2021 na 2022.
“Mpango Mkakati huu unalenga kutokomeza vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono ifikapo 2022 ili kusudi wanafunzi wa kike wanaosoma elimu ya juu waweze kufanikisha malengo yao bila kuwepo vikwazo kama vya kuombwa rushwa ya ngono” amesisitza Dk. Jingu.
Aidha Dkt. Jingu amewataka wakuu wa vyuo hao kuhakikisha wanatoa elimu na maelekezo ili kujenga uelewa wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanafunzi wa kike kwa kwa ajili ya kuepuka matakwa ya wahadhiri wanaotumia hila kuendekeza ukatili wa kingono vyuoni.
Pia Dkt. Jingu amewataka Wakuu wa vyuo hao kuhakikisha wanatekeleza Agizo la Waziri Ummy Mwalimu la kuanzisha madawati ya jinsia katika vyuo vyao ili kuwezesha kuondokana na vitendo vya kikatili na kujenga mazingira yaliyosalama katika vyuo vyetu.
Kwa upande wake Mkuu wa Uelimishaji kutoka Taasisi ya Kupambana na Kutokomeza Rushwa TAKUKURU Bw. Asseri Mandari amesema kuwa Taasisi hiyo imejipanga kupamabana na tatizo hilo kwa kuanzisha Kampeni inayaosema “Vunja Ukimya Ondoa Rushwa ya Ngono” itakayosaidia kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kuzuia rushwa ya ngono.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Jinsia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dkt. Lulu Mahai amesema kuwa Vyuo vya elimu ya juu vinawajibu mkubwa wa kuhakikisha wanatoa elimu kuhsu kupambana na vitendo vya kikatili kwa wanafunzi wa wafanyakazi na wanaamini baada ya kikao hiki watarudi na kuanzisha madawati ya jinsia na kamati mbalimbali zitakazosaidia kupambana na matukio ya ukatili wa kijinsia katika Taasisi na Vyuo vyote nchini.