********************************
Desemba 23, 2019. Dar es Salaam. Kampuni ya Vodacom Tanzania PLC imeongeza muda wa kufanya kazi katika maduka zaidi ya 400 ya Vodashop na madawati ya
huduma kwa Mteja (Customer Service Desk) nchini kote ili kukidhi mahitaji ya wateja wake ya kusajili laini za simu kwa alama za vidole kabla ya kufikia ukomo Desemba
31 mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC – Hisham Hendi alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa wateja wote wa Vodacom wanatekeleza matakwa ya
kusajili laini zao za simu kwa kutumia alama za vidole ili kuendelea kupata huduma ya mawasiliano.
“Tumeongeza saa zetu za kazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa mbili usiku. Hivyo wateja wetu wenye vitambulisho vya Taifa au namba ya kitambulisho cha Taifa watembelee maduka yetu katika kila kona ya nchi ili kusajili laini zao za simu. Hii itawawezesha kuendana na matakwa ya Serikali na kuwaondolea usumbufu wa kukosa mawasiliano, hasa katika msimu huu wa sikukuu ambapo kila mtu anahitaji kuwasiliana na ndugu, jamaa, marafiki na watu wake muhimu. Pia tunawashauri
wateja ambao hawajaomba kitambulisho cha Taifa wafanye hivyo haraka ili kukamilisha mchakato wa usajili wa laini zao,” alisema Hendi.
Aliongeza kuwa mawakala wa Vodacom wenye vitambulisho na mavazi maalumu watapita katika maeneo mbalimbali ya makazi, ofisi na biashara kuwezesha wateja
kusajili laini zao za simu.
Usajili wa laini za simu kwa njia ya alama za vidole unalenga kupunguza matumizi mabaya ya simu za kiganjani na kuongeza usalama.
Watanzania wanatakiwa kuwa na kitambulisho cha Taifa au namba ya kitambulisho hicho ili kukidhi mahitaji ya usajili huo. Kwa mujibu wa agizo la Serikali, laini zote za simu ambazo hazitasajiliwa kufikia Desemba 31 mwaka huu zitafungiwa.
“Sio lazima kuwa na kitambulisho cha taifa. Kama mtu anaweza kukumbuka nambari yake ya kitambulisho cha taifa (NIN) tunamsajili,” alifafanua Hisham.
Mapema mwaka huu, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitoa agizo kwamba laini zote za simu nchini zinatakiwa kusajiliwa katika mfumo wa alama za vidole. Mfumo wa utambuzi kwa kutumia alama za mwili (Biometrics) unatumika zaidi kama njia mojawapo ya kuwafahamu wateja (know your customer – KYC) ili kuzuia utapeli miongoni mwa wateja, hasa wale wa mitandao ya simu.