Mchungaji Mwenyeji wa Kongamano la Kwanza la Ndoa 2019, Dkt.Sako Mayrick, akitoa mada kuhusu kanuni 21 za ndoa yenye mafanikio na utajiri na maswali magumu katika kongamano hilo lililofanyika jana.
Mtume Paul Toritseju (kulia) kutoka Nigeria akizungumza wakati akitoa mada katika Kongamano la Kwanza la Ndoa 2019 kuhusu kanuni za kupata mwenzi na misingi ya ndoa yenye mafanikio lililofanyika jana Mnazimmoja, jijini Dar es Salaam. Kushoto, Mchungaji Mwenyeji wa Kongamano hilo, Dkt.Sako Mayrick. Kongamano hilo liliandaliwa na Success Chapel.
Mama Mchungaji Mariam Sako (kushoto) , akizungumza kwenye kongamano hilo. Kulia ni Hellen Sako.
Maombi yakifanyika katika kongamano hilo.
Mwezeshaji wa semina hiyo, Mchungaji Dkt. Robert Mbelwa akilitoa mada kuhusu lugha za ndoa kwa ajili ya mafanikio.
Picha ya pamoja.
Na Dotto Mwaibale
JAMII imeshauriwa kuacha tabia ya kuandaa sherehe za ndoa badala yake wajikite zaidi katika kuiandaa ndoa jambo litakalosaidia kupunguza changamoto ya ndoa nyingi kuvunjika.
Wito huo umetolewa na Mtume Paul Toritseju kutoka Nigeria wakati akitoa mada katika Kongamano la Kwanza la Ndoa 2019 lililoandaliwa na Success Chapel kuhusu kanuni za kupata mwenzi na misingi ya ndoa yenye mafanikio lililofanyika jana Mnazimmoja, jijini Dar es Salaam.
“Ndoa nyingi zimekuwa zikivunjika kwa sababu ya kukosa maandalizi kwa wahusika kutumia muda mwingi na fedha nyingi kwa ajili ya kuandaa sherehe badala ya ndoa” alisema Toritseju.
Alisema vijana wanatakiwa kujiandaa kwa ndoa waache kufikiria sherehe ambazo hazina msingi wowote na kuwa ndoa njema nikuwa katikati ya Mungu na kuwa ni uokozi.
Toritseju aliwataka vijana walio kwenye ndoa kuacha kukwepa majukumu na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na kuacha tabia ya masuala yao ya ndani kuwaeleza wazazi wao hasa mama kwani ndoa ni ya watu wawili wa jinsia mbili tofauti ya kike na kiume ambao wamekubaliana kuishi na kuwa mwili mmoja na si vinginevyo.
Mwezeshaji mwingine katika semina hiyo, Mchungaji Dkt. Robert Mbelwa akilitoa mada kuhusu lugha za ndoa kwa ajili ya mafanikio alisema ndoa ni taasisi ya kiroho na wala sio ya serikali, kisiasa na kidini hivyo inapaswa kuheshimiwa na watu wote.
” Ili ufanikiwe katika ndoa ni lazima uwe mcha Mungu na kuwa Mungu ndiye mwanzilishi wa ndoa” alisema Dkt.Mbelwa.
Alitaja mambo kadhaa ambayo yanatakiwa kuzingatiwa kabla ya kijana hajaoa au kuolewa kuwa ni pamoja na kuangalia elimu, maumbile, utajiri na mengine kwani kijana mwenye elimu ya darasa la saba akimuoa mke mwenye PhD ndoa hiyo haitadumu huko mbele wataanza kudharauliana.
Akizungumzia maumbile alisema hilo pia ni jambo la kuzingatia hauwezi ukawa mfupi ukaoa mwanamke mrefu hivyo walau kuwepo na kuzingatia maumbile yanayoendana.
Dkt.Mbelwa alishauri vijana kabla ya kuoa au kuolewa wafuate misingi iliyobora na si uzuri wa mtu kama vile ni kijana mtanashati au kwa kuwa ana matiti madogo, makalio makubwa na kadharika kwani vitu hivyo siku za mbeleni vinaweza kutoweka kwa sababu ya kuzeeka.
Mwenyeji wa Kongamano hilo la Kwanza la Ndoa, 2019, Mchungaji Dkt. Sako Mayrick akitoa mada kuhusu kanuni 21 za ndoa yenye mafanikio na utajiri na maswali magumu alisema mtu anapooa au kuolewa si kwa ajili ya kufanya ngono bali ni kumpata msaidizi wa maisha yake.
Alisema kunatofauti kubwa kati ya ngono, mapenzi na tendo la ndoa na kuwa ngono ni kufanya mapenzi hovyo hovyo kama wafanyavyo makahaba na mapenzi ni kumpenda mtu yeyote kama mzazi au rafiki na tendo la ndoa ni tendo takatifu linalofanywa na wanandoa kwa ajili ya kuwafanya wawe karibu.