Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma Grace Quintine wakwanza kulia akiwa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa RUVUMA,Halmashauri Mji Mbinga imepongezwa na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tamisemi Seleman Jafo kwa usimamizi na matumizi sahihi ya fedha za miradi ya maendeleo zinazopelekwa katika Halmashauri hiyo.
…………………….
Na Mwandishi WETU,Mbinga
WAZIRI wa Nchi ofisi ya Rais Tamisemi Seleman Jafo,amemuagiza mkandarasi Suma Jkt anayejenga jengo la ofisi za Halmashauri ya mji Mbinga mkoani Ruvuma, awe amekamilisha kazi hiyo ifikapo tarehe 30 Desemba mwaka huu.
Halmashauri ya Mji Mbinga,imeingia mkataba na Suma JKT kujenga jengo hilo lenye ghorofa moja kwa gharama ya shilingi bilioni 2.9 mwaka 2018 ili kurahisisha utoaji huduma na kuwaondolea adha watumishi wa Halmashauri hiyo, ambao kwa sasa wanalazimika kubanana katika jengo la idara ya ujenzi walilorithi kutoka halmashauri ya wilaya Mbinga.
Aidha Waziri Jafo, amezitaka wa Halmashauri nyingine za mkoa wa Ruvuma,kuiga mfano wa Halmashauri ya mji Mbinga kwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa jengo hilo sambamba na matumizi mazuri ya fedha zinazopelekwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuchochea na kuharasisha maendeleo.
Waziri Jafo ametoka kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akikagua ujenzi wa jengo la ofisi za Halmashauri hiyo na kuwataka wakurugenzi wengine wa mkoa wa Ruvuma kuiga utendaji, na uadilifu wa Mkurugenzi wa Mji Mbinga Grace Quintine na timu yake.
“lazima wakurugenzi wengine waige mfano mzuri wa Mbinga Mji, ukipewa fedha basi uzitumie vizuri,Mheshimiwa Rais ametafuta fedha za kujenga jengo hili ili watumishi mfanye kazi zenu katika mazingira bora, Mkuu wa mkoa hapa nimeridhika na kazi iliyofanyika,kwa kweli nimefurahi sana kwani fedha zilizoletwa zimefanya kazi nzuri nampongeza Mkurugenzi na watu wake”alisema Waziri Jafo.
Waziri Jafo alisema, baadhi ya maeneo zinapelekwa fedha lakini hakuna kazi zinazofanyika badala yake kunakuwa ubabaishaji mkubwa unaokwamisha na kuchelewesha mipango ya Serikali.
Ameitak Suma Jkt kufanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha jengo hilo linaanza kutumika kabla ya mwisho wa mwezi Januari 2020 kwa kuwa mkataba wake ni Mwezi Desemba 2019 na imani yake kuwa watumishi watahami katika jengo hilo mapema.
Kwa upande wake mhandisi anayesimamia ujenzi wa jengo hilo Amos Agostine alisema, ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 95 na kwamba gharama za ujenzi ni zaidi ya Bilioni 2,983,122,246.
Amos alisema, kwa sasa wapo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi huo kwa kupaka rangi,kuunganisha umeme,kujenga ngazi na shughuli nyingine ndogo ndogo.