Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh.Seleman Jafo (Mb)(katikati),akizungumza na wananchi( hawapo pichani) na viongozi wa Mkoa na Wilaya ya Nyasa, alipokuwa anakagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa iliyojengwa katika kijiji cha Nangombo Kata ya kilosa Wilayani Nyasa Mkoani Ruvuma, akiwa katika ziara ya siku moja ya kikazi ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo, inayosimamiwa na ofisi yake kulia kwake ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Bi
chiristina Mndeme na kushoto kwake ni Mbunge wa Nyasa Mhandisi Stella Manyanya.(Picha na Ofisi ya Mkurugenzi wa wilaya ya Nyasa)
*******************************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh.Seleman Jafo (Mb), jana ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma kwa
kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa kwa wakati uliopangwa.
Alizitoa pongezi hizo jana alipokuwa katika Ziara ya kikazi ya siku moja ya kutembelea na kukagua, miradi ya maendeleo inayosimamiwa na ofisi yake katika Wilaya ya Nyasa.
Bw.Jafo alifafanua kuwa ameridhishwa na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa, kwa kuwa imejengwa vizuri na kwa ubora wa hali ya juu. Hivyo aliwapongeza viongozi,wa Wilaya ya Nyasa na wananchi kwa ujumla kwa kushirikiana, na kusimamia vema ujenzi wa Hospitali hiyo, na kukamilisha kwa wakati licha ya umbali uliopo ukifananishwa na sehemu zingine.
“Nachukua fursa hii kuwapongeza sana Viongozi na wananchi wote wa Wilaya ya Nyasa kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Hospitali hii kwa kuwa imejengwa kwa ubora
ukilinganishwa na umbali wa kijiografia kwa kuwa Wilaya ya nyasa iko Mbali ikilinganishwa na Wilaya zingine”.
Aidha aliwataka wananchi hao watambue kwamba ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na vituo vingine vya Afya, ujenzi wa miundombinu ya shule, na ujenzi wa barabara ya
Lami kutoka Mbinga hadi MBamba-bay ni upendo wa moyoni wa Mh. Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuwa ameamua kutatua kero za Wananchi wa Wilaya ya nyasa na Tanzania kwa ujumla hasa Wanyonge.
Alitoa wito kwa wananchi kuitunza miundombinu ya majengo ili iweze kutumika kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya alimuomba Waziri Jafo kuwaongeza watumishi wa Afya katika Wilaya ya Nyasa ili Hospitali hiyo ianze kufanya kazi.
Wilaya ya Nyasa imepewa na Serikali jumla ya Shilingi bilioni moja na nusu kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Nyasa na inatarajia kutatua kero ya wananchi wa Wilaya ya Nyasa waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilometa 66 kufuata matibabu katika hospitali ya wilaya ya Mbinga na Hospitali ya Mkoa Songea.