Na.Farida Saidy,Morogoro
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewataka wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali za kibinadamu jirani na miundombinu ya umeme kuacha mara moja ili kujiepusha na madhara yatakayotokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na fullshangwe blog, Kaimu Meneja Mahusiano TANESCO, Leila Muhaji amesema wale wote wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo kuegesha magari,kulima,kujenga makazi ya kuishi, na kufanya biashara katika miundombinu ya umeme wanatakiwa kuacha.
Amewatahadharisha wananchi kutoshika au kukanyaga nyaya za umeme zilizoanguka hususan katika kipindi hiki cha mvua.
“Ni vyema kutoa taarifa Tanesco kitengo cha dharura kwa msaada zaidi,”amesema.
Katika hatua nyingine amesema kuwa iwapo mvua itaambatana na radi upepo mkali au umeme utapungua nguvu na kuongezeka ndani ya nyumba hivyo wananchi wanashauriwa kuzima umeme kwenye ‘Main switch’, ili kuepukana na majanga yatokanayo na shoti ya umeme.