Kutokana na uwepo wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha karibu mikoa yote hapa nchini na mvua kusababisha mito kujaa sana na maji kuwa na kasi kubwa. Hivyo baadhi ya sehemu maji hufurika na kufunika madaraja na makaravati.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linawatahadharisha wananchi kutothubutu kujaribu kuvuka kwenye madaraja au makaravati yaliyofunikwa na maji, kuna uwezekano mkubwa daraja au karavati kusombwa na maji. Aidha madereva wasijaribu kuvusha vyombo wanavyoendesha maana ni hatari kufanya hivyo.
Kuvuka maeneo kama hayo kunaweza kuleta maafa makubwa kwa jamii ikiwemo kupoteza maisha kwa kusombwa na maji. Hivyo wasubiri mpaka maji yatakapopungua kiasi kwamba daraja au karavati vinaonekana vizuri na ni salama kuvuka, pia watu wasitembee kwenye kingo za mito, maana kingo za mito huwa dhaifu kutokana na ardhi kujaa maji.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limejipanga na liko imara kuhakikisha linatoa huduma bora, sahihi na kwa wakati. Hivyo wananchi mnapoona janga lolote tafadhali toeni taarifa mapema kwa kupiga namba ya dharura 114.