Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua shamba la mifugo mara baada ya kutembelea Chuo cha Kilimo cha Uyole (MATI Uyole) wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya, tarehe 21 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na Uongozi na wanafunzi wa Chuo cha Kilimo cha Uyole (MATI Uyole) wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya, tarehe 21 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua maabara ya udongo mara baada ya kutembelea Chuo cha Kilimo cha Uyole (MATI Uyole) wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya, tarehe 21 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na Uongozi na wanafunzi wa Chuo cha Kilimo cha Uyole (MATI Uyole) wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya, tarehe 21 Disemba 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua eneo linalozalisha miche ya mikorosho mara baada ya kutembelea Chuo cha Kilimo cha Uyole (MATI Uyole) wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya, tarehe 21 Disemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
…………………………………………………..
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya
Serikali imeeleza dhamira yake ya kukarabati vyuo vyote vya kilimo nchini ili kukabiliana na changamoto zinazovikabili vyuo hivyo ambapo ni pamoja na uchache na uchakavu wa vitendea kazi kama maabara, vifaa vya TEHAMA, na zana za kilimo yakiwemo matrekta.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 21 Disemba 2019 wakati alipotembelea Chuo cha Kilimo cha Uyole (MATI Uyole) wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya.
Ameeleza kuwa dhamira ya kukarabati vyuo hivyo imetokana na kujionea uchakavu wa miundombinu ikiwemo barabara, mifumo ya maji, majengo (Mabweni na nyumba za watumishi) katika chuo hicho pamoja na vyuo vingine vya kilimo.
Amesema kuwa serikali itakarabati vyuo hivyo ili kuwa na vyuo vya kisasa vinavyopendeza na vitakavyokuwa chachu ya kupata wataalamu waliokomaa kupitia mitaala iliyoboreshwa na zana bora za kilimo.
Pia, Mhe Hasunga amesema kuwa ili kuwa na wataalamu waliobobea vizuri kwenye sekta ya kilimo wizara yake imekusudia kuongeza muda wa mafunzo kwa vitendo (Field) kufikia mwaka mmoja kwani kufanya hivyo kutaongeza msukumo na kumjengea uwezo mkubwa mwanafunzi.
“Tutafanya hivyo ili kuona alichojifunza mwanafunzi kama kina akisi weledi katika jamii na kama wazo hilo likikubalika tutarekebisha mitaala yetu ya kufundishia katika vyuo vyote vya kilimo na vyuo vikuu” Alikaririwa Mhe Hasunga
Kadhalika, Waziri Hasunga amewaagiza wakufunzi wa chuo cha kilimo cha Uyole (MATI Uyole) kuhakikisha kuwa wanaandika vitabu na majarida mbalimbali kwani maarifa na ujuzi walionao utasaidia kuhakikisha kuwa kile walichonacho kinawafikia watu wengi zaidi.
Amesema kuwa machapisho na vitabu watakavyoandika vitasaidia katika siku za usoni wanafunzi kuweza kujifunza na kuona umuhimu wa kuandika vitabu ama majarida.
Waziri Hasunga ameongeza kuwa wizara ya kilimo inaendelea kufanya Mabadiliko ya kisera na kisheria ili kuimarisha sekta ya kilimo na wakulima nchini kuondokana na dhana ya kilimo cha kujikimu na kuwa na kilimo cha kibiashara.
Ameongeza kuwa dhamira kubwa kabisa ni pamoja na kuwa na kilimo chenye uwezo wa kutoa ajira na mchango mkubwa katika sekta ya viwanda na kuongeza fedha za kigeni.
“Sasa ili kufikia kilimo cha namna hiyo kuwa na utitiri wa Bodi inaonekana usimamizi wake kupwaya hivyo tunakusudia katika mabadiliko hayo kuziunganisha bodi zote na kuwa na Bodi tatu pekee” Alisema
Waziri Hasunga ameongeza kuwa tayari kamati maalumu ya wataalamu imetuama Jijini Dodoma ili kutathmini vyuo 14 vya kilimo vilivyopo, vituo 17 vya utafiti na vingine vidogo 23 ili kubaini kiasi mahususi kinachohitajika ili kufanya maboresho ya vyuo hivyo.