MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Mhe.Asha Abdulla Juma akikabidhi Vifaa vikiwemo vitambaa pamoja na Vyerehani kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania Wilaya ya Mjini Habiba Nassib Suleiman kwa ajili ya Kituo cha Elimu Amali UWT Wilaya ya Mjini.
………………………………………………..
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
MBUNGE wa viti maalum wa mkoa wa Mjini,Asha Abdullah Juma amefurahishwa na hatua ya Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) ya Chama Cha Mapinduzi ya wilaya ya Mjini kutekeleza kwa vitendo ilani ya uchaguzi kwa kuhakikisha vijana wanajikwamua kiuchumi.
Amesema kitendo cha UWT kuwakusanya vijana tofauti ndani ya mkoa huo kwa lengo la kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kuondokana na hali ya utegemezi ambapo baadaye wakipata ujuzi wanajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ili kujiingizia kipato ni moja ya sehemu ya maagizo ya ilani pamoja na viongozi wa chama.
Kauli hiyo ameitoa wakati akikabidhi vifaa vya ushonaji ikiwemo chereheani mbili,meza pamoja na vitambaa vya kutengeneza mapambo katika kituo cha mafunzo ya amali cha UWT wilaya ya mjini ambapo alisema hiyo ni ahadi za CCM katika kuwakusanya vijana na kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kuondokana na utegemezi.
Alisema baada ya kuona Jumuiya hiyo imeanzisha kituo hicho cha mafunzo kwa ajili ya vijana akaiona aunge mkono juhudi hizo za kuhakikisha vijana hao wanaokombolewa dhidi ya ukosefu wa ajira ili kuongeza uzalishaji nchini kama maagizo ya viongozi wa CCM wanavyoelekeza.
“Nina amini chuo hichi kitasaidia sana juhudi hizi kwa vijana wetu na ndio maana nikaona nilete nguvu kwenye kituo hichi cha UWT hasa kwa wakina mama katika kujifunza ujasiriamali wa ushonaji,upishi na mambo mengine,”alisema
Naye Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Mjini,Habiba Nassir Suleiman alisema azma ya uongozi wa wilaya hiyo ya jumuiya hiyo ni kubuni miradi itakayosaidia kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira na ongezeko la uzalishaji kwa lengo la kukuza uchumi kama inavyoelekeza CCM.
Alisema uongozi wa UWT wilaya imeamua kufanya ubunifu wa aina hiyo wa kuwakusanya vijana na kuwapatia mafunzo ya ujuzi wa shughuli za ujasiriamali ambapo kwa namna moja ama nyingine itawasaidia sana wanawake katika kuondokana na hali ya utegemezi na kuweza kujikwamua kiuchumi.