**************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
JUMLA ya wanafunzi 184 wamepata mimba mkoani Pwani, ambapo wa sekondari wakiwa ni 144 na wale wa shule za msingi ni 40 katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba mwaka huu.
Pamoja na hilo,mkoa huo umewalipa wakulima wa zao la korosho kiasi cha sh.bilioni 60.6 kwa msimu wa mwaka 2018/2019
Akielezea suala la mimba za utotoni, mjini Kibaha na Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa kikao cha Ushauri ya Mkoa (RCC) alisema katika kukabiliana na hali hiyo lazima wazazi na wadau mbalimbali waweke mikakati ya kukabili changamoto hiyo.
Alifafanua, kwa mwaka huu ufaulu umeongezeka ambapo jumla ya wanafunzi waliofanya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi walikuwa 29,914 na waliofaulu walikuwa 25,465.
“Kutokana na ufaulu huu mkoa unakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 59 ambapo wanafunzi 2,918 watakosa nafasi za kwenda sekondari moja kwa moja itabidi wasubiri hadi vyumba hivyo vitakapokuwa vimekamilika ifikapo Januari 30 mwakani,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa wanafunzi hao ni kutoka kwenye halmashauri za Chalinze,Kisarawe na Mkuranga huku Halmashauri tisa zikiwa zimepeleka wanafunzi moja kwa moja.
“Kama tulivyokubaliana halmashauri zihakikishe zinakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili ikifika mwakani vyumba hivyo viwe vimekamilika ili wanafunzi waliokosa nafasi wawahi masomo,” alisema Ndikilo.
Akizungumzia kilimo cha korosho ,alieleza licha ya kulipa wakulima wa zao hilo sh.bilioni 60.6 ,korosho daraja la kwanza ziliuzwa kwa sh.2,571 na daraja la pili ziliuzwa kwa sh. 2,075 ambapo hadi Desemba jumla ya tani 765 zimeuzwa.
Alieleza kwa wakulima ambao hawajalipwa serikali inaendelea na uhakiki .
“Korosho itakayolipwa ni ile itakayokuwa imepelekwa kwenye ghala kuu lakini zile zilizo kwenye vyama vya msingi vya ushirika watalipwa huko huko,” alisema Ndikilo.
Alieleza, hadi sasa kuna tani zaidi ya 6,000 ziko kwenye vyama vya ushirika vya msingi Amcos na korosho nyingine ziliharibika kutokana hali ya mvua na ukosefu wa magunia.