**********************************
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga amepongeza juhudi zinazofanywa na watumishi kituo cha afya cha Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga baada ya kuona namna wanavyokabiliana na ongezeko la wateja wanaohitaji huduma za afya katika kituo hicho ambacho huzalisha wajawazito wapatao 373 kwa mwezi.
Amesema kuwa kabla ya hapo kituo hicho kilikuwa kidogo sana na kushindwa hata kutoa huduma za upasuaji jambo ambalo lilipelekea hospitali ya rufaa ya mkoa kuzidiwa na wagonjwa lakini hali hiyo kwa sasa ni tofauti baada ya upanuzi wa kituo hicho ambacho kutokana na huduma zake wateja wengi huvutiwa kufika na kupata huduma.
Amesema kuwa serikali inatoa fedha nyingi kupata dawa pamoja na vifaa tiba hivyo kinachotegemewa katika kituo hicho ni huduma bora ya afya na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imejenga vituo vya afya zaidi ya 352 ambapo mojawapo ya vituo hivyo ni kituo cha afya cha Mazwi katika Makispaa ya Sumbawanga ambapo walipatiwa shilingi milioni 500 na sasa kituo hicho kimekamilika na kuanza kutoa huduma.
“Nimefurahishwa kwa upanuzi ambao umefanyika katika kituo hiki cha Mazwi, kilikuwa kituo kidogo tu nakumbuka siku za nyuma lakini kimekarabatiwa kimekuwa kituo kizuri na kinapendeza lakini kitu cha kufurahisha ni kwamba kinahudumia wateja wengi lakini na huduma inayotolewa hapa nimetoka kukagua katika maeneo mbalimbali katika wodi kwakweli nimeridhika na huduma ambazo zinatolewa, changamoto ni kwamba wameongezeka wateja baada ya ukarabati kufanyika, tunashukuru wataalamu wetu wanajitahidi kuwahudumia,” Alisema.
Wakati akitoa taarifa ya kituo cha Afya cha Mazwi Mganga Mkuu wa halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga Dkt. Archie Hellar alisema kuwa kuanzia mwezi Januari hadi Novemba kituo hicho cha afya kimezalisha wajawazito 4,103 na kati ya hao waliofanyiwa upasuaji ni wajawazito 426 na kupatikana vifo viwili kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo katika harakati za kuwafanyia wajawazito hao upasuaji.
“Kwajhiyo changamoto tunazozipata ni kwamba wateja ni wengi zaidi wanaichukulia hospitali hii ni kama ya mkoa na wengine wanatoka nje ya manispaa n ahata nje ya Wilaya nyingine kuja kujifungua hapa, sasa ukilinganisha watumishi pamoja na rasilimali fedha unakuta kituo kinaelemewa, lakini hata hivyo tunajitahidi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wetu wa manispaa Jacob Mtalitinya kwakweli anatiupa nguvu na kutusaidia sana kufanikisha kutoa huduma,” Alisema.
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ilipata shilingi milioni 500 za kupanua ujenzi wa kituo cha Afya cha Mazwi pamoja na kupewa shilingi milioni 400 kwaajili ya ujenzi wa kituo cha Afya kipya kilichopo katika kata ya Katumba azimio ikiwa ni kilometa 12 kutoka katika kituo cha afya cha Mazwi.