*************************************
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamuhanga amesema kuwa Ofisi ya Rais inaendelea kufanya tathmini kwa hospitali zote 67 kuhakikisha kwamba shilingi bilioni 100.5 ambazo zilitolewa kwa ujenzi wa hospitali hizo kuwa zimetumika vizuri.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imejenga hospitali 67 nchini na mkoa wa Rukwa umejengewa hospitali tatu za wilaya ambapo Mhandisi Nyamuhanga aliweza kutembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kalamnbo, katika mji mdogo wa Matai iliyopokea shilingi Bilioni 1.5 lakini hakuridhishwa na ujenzi wa hospitali hiyo.
“Kwa halmashauri ambazo fedha hizi zitakuwa hazijatumika vizuri kwakweli tutachukua hatua na katibu tawala wa mkoa kama nilivyoagiza jana, najua kuna vifaa ambavyo tayari vimeshanunuliwa pale ambavyo bado havijawekwa, havijajengwa kwa mfano maru maru na vifaa vingine uhakikishe kwamba kazi hiyo inaendelea ili vifaa hivyo vikishawekwa tuvitathmini sasa kiwango cha ukamilishaji wa hospitali ile ya halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kabla hatujafikiria kutoa fedha nyingine za kukamilisha,” Alisema.
Ameongeza kuwa halmashauri hiyo ya Kalambo imetaja mahitaji ya shilingi milioni 700 ili kuweza kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo jambo ambalo Mhandisi Nyamuhanga hakukubaliana nalo kutokana na tathmini iliyofanywa ya mahitaji ya fedha walizotoa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hizo kuwa yangebaki mambo machache ambayo yasingeweza kuzidi shilingi milioni 300 na kuongeza kuwa anahitaji maelezo ya ziada kutoka katika halmashauri hiyo ambayo hospitali yake imefikia ukamilifu wa asilimia 76 ambacho ni kiwango cha chini cha ukamilishaji.
Katika hatua nyingine amesema kuwa mwezi Aprili mwaka 2019 Ofisi ya Rais TAMISEMI ilitoa shilingi milioni 400 kwaajili ya upanuzi wa Zahanati ya Kijiji cha Samazi katika halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ambapo zahanati hiyo inapandishwa hadhi na kuwa kituo cha Afya lakini amesikitishwa na malumbano yanayoendelea katika kijiji hicho juu ya eneo la ujenzi wa kituo hicho jambo lililopelekea kushindwa kuanza kwa ujenzi huo.
“Ofisi ya Rais TAMISEMI imetoa maelekezo kwamba upanuzi ufanyike katika eneo la zahanati iliyopo iongezewe majengo ili kiwe kituo cha afya cha Samazi kiweze kukamilika ili kiweze kufanya kazi, tusiendelee na malumbano tena tumeshatoa maamuzi kwamba upanuzi ufanyike pale kwenye zahanati ili tukipandishe hadhi ikiwe kituo cha afya, tunategemea kazi hiyo ianze mara moja na ikamilike ndani ya miezi mitatu,” Alisisitiza