…………….
Na Boniphace Richard ,Dodoma
Serikali imesema taarifa ya ripoti ya maendeleo ya binadamu kwa mwaka 2019 imeonyesha matumaini ya kukua kwa uchumi wa nchi pamoja na maendeleo mengine kwa ujumla.
Akizindua ripoti hiyo jijini Dodoma leo, Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Prof Adolf Mkenda amesema matumaini hayo ya kukua kwa uchumi kwa kasi yametokana na jitahada za uwekezaji kwenye sekta ya afya na elimu ambapo kumechangia kupanda kwa wastani wa maisha ya mtanzania hadi kufikia miaka 65.
“juhudi za serikali zimeanza kuzaa matunda” alisema Mkenda
Aidha kwa upande wake mwakilishi kutoka shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) bi. Christine Musisi, amesema wananchi watapata taarifa zaidi kupitia ripoti hiyo kutoka kwa wachambuzi ambapo ripoti hiyo inazungumzia uhusika katika mazingira ya Tanzania zaidi.
Pamoja na hayo, mkuu wa mkoa wa Simiyu bw. Anthony Mtaka amesema mapinduzi katika sekta ya elimu yametoa nafasi kubwa kwa makundi ya watanzania kwenda shule.
“ sasa huko tunakoenda tunaenda kuwa na Tanzania yenye changamoto ya ajira hususani ajira za vijana wasomi na wenye ujuzi”
Pia ameongeza kuwa, kusekana kwa usawa wa kidunia kumegawanyika katika makundi mengi ikiwemo, kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na makundi ya rika ambapo makundi lengwa yamekuwa ya watoto, vijana na makundi ya kina mama.
Kiujumla ripoti ya maendeleo ya binadamu inatoa nafasi kwa viongozi kutathimini maisha yajayo ya jamii inayotuzunguka hususani kizazi kijacho, pia ni lazima watunga sera pamoja na watenda maamuzi kuangazia tanzania ya kesho kutwa.
“Huko nyuma tulikuwa na kundi kubwa la watanzania ambao hawana ajira lakini hawajasoma ni wakati ambao tulikuwa na watu wengi wa darasa la saba watu wengi hawajaenda shule” alisema Mtaka
Taarifa ya leo inatoa elimu kwa viongozi na taifa kwa ujumla kuchagua ni aina gani ya kiongozi ambae anafaa katika maamuzi ya kutunga sera haswaa kipindi hiki cha uchaguzi mkuu 2020, ambapo ni lazima jamii iamue inahitaji kiongozi wa aina gani ikiwa ni pamoja na kuchagua mkuu wa mkoa, diwani, mkuu wa wilaya, pamoja na mkurugenzi wa aina gani ambae atafaa kwenye dunia ambayo tunaelekea.