Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA hususan wapenzi wa filamu nchini sasa watanufaika na huduma ya ‘T-Burudani’ toka TTCL itakayomwezesha mteja kupakua, kuhifadhi pamoja na kuangalia filamu aipendayo bila ya kuwa na mtandao wa intaneti
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, kutambulisha huduma hiyo ambayo kwa sasa inatolewa bure, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Waziri Kindamba alisema kampuni hiyo imeamua kutoa zawadi ya T-Burudani kwa wateja wake hasa wapenzi wa filamu.
“T-BURUDANI ni huduma itolewayo na TTCL itakayomuwezesha mteja kupakua filamu bila kutumia kifurushi cha intaneti, mteja ataweza kuangalia filamu zote za ndani ya nchi pamoja na kimataifa. Huduma hii mteja ataweza kupakua kupitia simu janja ya mkononi pamoja na kompyuta ya kiganjani ‘Tablet’,” alisema Bw. Kindamba.
Akifafanua zaidi Kindamba alisema TTCL katika huduma hiyo imeweka mfumo rahisi utakaomuwezesha, mteja kupakua filamu aitakayo kutokana na maudhui toka kote duniani pamoja na Hollywood, Nollywood, Bollywood, HBO, hata Bongo movies.
Aidha aliongeza kuwa mteja ataweza kuangalia kwa kipindi atakachohitaji lakini vile vile ataweza kupakua na kuhifadhi kwa gharama nafuu kupitia ‘App’. Sanjari na huduma hiyo alibainisha TTCL imeamua kuwafuata wateja wake maeneo yao kwa kuwatakia heri na sikukuu kupita kampeni yake ijulikanayo kama MTAA KWA MTAA, pia kuwahudumia zaidi.
“Zawadi hii ni kwa wateja wetu wa TTCL ni kwa gharama nafuu sana ambapo kuna kifurushi kwa shilingi elfu moja kwa siku,elfu tatu kwa siku saba na shilingi elfu tano kwa mwezi mzima. Hakika hii ni burudani tosha kwa watanzania. Mteja ataweza kupata huduma hii kwa kupitia T-Burudani App ambayo inapatikana katika ‘playstore’ na ‘App store’. Aidha nitangaze rasmi kwa sasa bidhaa hii ni bure kabisa pasipo na malipo yoyote mpaka tarehe 31 Desemba,” alisema.
“Nichukue fursa hii kuwatangazia rasmi wateja wetu bidhaa hii ni bure kwa muda maalumu hasa katika kuwashukuru wateja wetu kwa kuwa nasi kwa kipindi cha mwaka mzima. T-Burudani ndio zawadi pekee na nono katika msimu huu wa sikukuu kulinganisha na watoa huduma wengine wa mawasiliamo. Tuendelee kufurahia kurudi Nyumbani kumezidi kunoga na T-Burudani.”
Hata hivyo alisema zawadi hiyo kwa wateja, inaenda sanjari na kampeni ya MTAA KWA MTAA inayolenga kuwatembelea Mawakala wao pamoja na wateja wa TTCL.