Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akikagua ujenzi tenki la maji la ujazo wa lita
50,000 la Mradi wa Maji wa Gwata katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini,
mkoani Morogoro.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Morogoro, Mhandisi Grace Lyimo akisoma taarifa
ya Mradi wa Maji wa Gwata uliopo katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini kwa
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.
Mkurugenzi wa Usambazaji Maji Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini
(RUWASA), Mhandisi Mkama Bwire akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Maji,
Jumaa Aweso.
Ujenzi wa tenki la maji la ujazo wa lita 50,000 la Mradi wa Maji wa Gwata ukiwa
katika asilimia 70 ya ujenzi katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini, mkoani
Morogoro.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Gwata akitoa malalamiko ya kero ya maji katika
kijiji hicho kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.
******************************************
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametoa onyo kali kwa wahandisi wa maji nchini kutoanza kazi yoyote ya ujenzi wa miundombinu ya miradi ya maji bila kupata chanzo
cha maji cha uhakika.
Onyo hilo limekuja baada ya kukagua Mradi wa Maji wa Gwata uliopo katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini, mkoani Morogoro na kukuta changamoto ya chanzo
cha maji cha Chalinze, mkoani Pwani kuwa kuwa kikwazo cha mradi huo kushindwa kutoa maji.
Taarifa ya mradi huo iliyosomwa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Morogoro, Mhandisi Grace Lyimo imeonyesha kuwa tatizo la chanzo tarajiwa kilichopo Chalinze, mkoani
Pwani kilichokuwa kitumike kushindwa kufikisha maji katika Kata ya Gwata licha ya kazi za ujenzi wa matenki mawili, vituo vya kuchotea maji na ulazaji wa mabomba ikiwa inakaribia kukamilika kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 261.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Gwata, Naibu Waziri Aweso amesikitishwa na kitendo hicho ambacho kimesababishwa na kukosewa kwa usanifu na kuitaka RUWASA kufika kwenye mradi huo kuuangalia, akisema kitaalam kosa hilo ni kubwa na hakutegemea kosa kama hilo lifanywe na watu wenye uwezo na kazi za uhandisi.
Akaielekeza TAKUKURU kuanza uchunguzi mara moja wa mradi huo, ikiwa ni pamoja na kuihoji Kampuni ya Don Consult iliyofanya usanifu wa mradi huo.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Usambazaji Maji Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Mkama Bwire amesema kiufundi mradi huo
umekosewa usanifu, hivyo watabaki Gwata pamoja na timu ya wataalam RUWASA kuupitia na kufanya usanifu upya ili uweze kukidhi mahitaji ya sasa pamoja na
kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu kutafuta chanzo mbadala kilicho karibu zaidi katika Mkoa wa Morogoro baadala ya Pwani.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alimwomba Naibu Waziri wa Maji kuupatia ufumbuzi haraka mradi huo uweze kukamilika kwa kuwa umechukua muda mrefu tangu ujenzi wake uanze, pamoja na wananchi kuwa na matumaini makubwa na
mradi huo kumaliza tatizo la maji linalowakabili.
Mradi wa Maji wa Gwata ulisanifiwa mwaka 2015 kwa lengo la kuhudumia wakazi 2,509 na ujenzi wake ulianza Julai, 2015 chini ya Mkandarasi, MS Kumba Quality Co. Ltd kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 440.