SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kupitia kampuni yake tanzu ya T-PESA imeingia makubaliano ya kibiashara na HaloPesa, ambapo kwa sasa wateja wa T-PESA wanaweza kutuma pesa kwenda Halopesa na vile vile wa Halopesa kutuma pesa kwenda T-Pesa.
Makubaliano hayo ya kibiashara yamesainiwa leo jijini Dar es Salaam, ambapo Mkuu wa Kitengo cha T-PESA, Bi. Lulu Mkudde ameiwakilisha T-PESA huku HaloPesa ikiwakilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Biashara, Bw. Magesa Wandwi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Mkudde alisema kupitia wakubaliano hayo kwa sasa mteja wa T-PESA ataweza kununua vifurushi, muda wa maongezi, kulipia bili na kufanya miamala mbalimbali kwenda taasisi zingine.
“Huduma hizi ni kwa wateja wote ambao wanatumia mtandao wa simu wa TTCL na pia kwa mtandao wa simu wa Halotel. Napenda kutumia fursa hii pia kuwapongeza ndugu zetu wa kampuni ya Halotel kwa kuunganisha taasisi kadhaa za umma kote nchini kwa kupitia ‘Optical Fiber’ na kuunganisha vijiji zaidi ya 1000 kwenye gridi ya mawasiliano ya simu ambayo hapo awali haikuhudumiwa,” alisema Bi. Mkudde.
Aidha aliongeza kuwa T-PESA ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) inazidi kuboresha huduma zake kwa wateja wake siku hadi siku nchi nzima.
Hata hivyo alibainisha uboreshaji huduma za T-Pesa umeleta ufanisi na kuongeza kwa matumizi ya miamala ya kieletronikia ambayo ni pamoja na uuzaji na ununuzi wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa njia za ki-elektroniki huku wakizingatia usalama na unafuu wa huduma.
T-PESA nikampuni ambayo imedhamiria na inatekeleza adhma ya kuwafikishia wananchi huduma za kifedha kwa njia za simu mahali walipo ili kuokoa muda wao ambao wanautumia kuzalisha na kukuza uchumi. T-PESA imekuwa kiungo muhimu cha kurahisisha shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo na biashara na pia ufikishaji wa huduma kwa wananchi zaidi ya milioni mbili walokuwa mjini na vijijini.
Mkuu wa Kitengo cha T-PESA, Lulu Mkudde (kulia) akizungumza katika hafla hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Halopesa, Bw. Magesa Wandwi. |
Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Halopesa, Bw. Magesa Wandwi (kushoto) akizungumza katika hafla hiyo. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha T-PESA, Lulu Mkudde. |