Home Mchanganyiko MDH WAZINDUA UPIMAJI WA KIFUA KIKUU KWA NJIA YA MPIRA RUVUMA

MDH WAZINDUA UPIMAJI WA KIFUA KIKUU KWA NJIA YA MPIRA RUVUMA

0
Na Mwandishi Wetu, Tunduru
SHIRIKA  la Usimamizi na Uboreshaji wa Huduma za Afya ngazi ya Jamii(MDH) kwa kushirikiana na Serikali,limezindua mpango wa uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa TB kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kwa njia ya mpira(mrija).
Uzinduzi huo umefanyika katika  zahanati mbili za Ligoma,Misechela  na Hospitali ya Misheni Mbesa na Hospitali ya wilaya Tunduru ambao ulikwenda sambamba na mafunzo  kwa vitendo ya kuwajengea uwezo  baadhi ya wauguzi na Madaktari  kutumia njia hiyo mpya kubaini vimelea vya ugonjwa huo kwa watoto.
Mkuu wa Program  na mafunzo wa MDH Dkt John  Lymo alisema,baada ya uzinduzi kufanyika katika wilaya ya Tunduru wataendelea na wilaya nyingine za mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuwabaini na kuwaanzishia dawa watoto wote watakaobainika kupatwa na maradhi ya kifua kikuu.
Dkt Lymo ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya watoto hapa nchini alisema,  lengo la  MDH ni kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutokomeza  kabisa ugonjwa wa kifua kikuu ifikapo mwaka 2030 na wapo katika mikoa minane hapa nchini ya Kagera,Mbeya,Dodoma,Tanga,Mara,Shinyanga na Simiyu.
Kwa mujibu wa Dkt Lymo,mpango huo ambao ni mpya hapa nchini utaleta tija kubwa  na utasaidia kuokoa maisha ya watoto wengi walio na umri chini ya miaka mitano kwani uzoefu unaonesha kuwa,watoto wadogo kila wanapokohoa  umeza makohozi,kwa hiyo inakuwa vigumu kwa wataalam kupata makohozi  kwa ajili ya kufanyia vipimo.
Alisema,uchunguzi wa vimelea vya TB kwa kutumia mpira ndiyo njia muafaka kwani mpira uingia moja kwa moja  tumboni ambako makohozi hayo yamejificha  na kusisitiza kuwa,njia hiyo ni  salama na sahihi kuibua ugonjwa huo kwa watoto ikilinganisha na watu wazima.
Alisema, ugonjwa wa kifua kikuu unatibika kwa mtu aliyepata  kuwahi Hospitali na kuanzishiwa dawa ambazo zinatolewa bure katika zahanati,vituo vya Afya na Hospitali zote hapa nchini.
Dkt Lymo, amewataka wazazi na walezi pindi wanapoona mabadiliko ya Afya kwa watoto wao ni vema kuwahi katika vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya uchunguzi.
Alisema, MDH inashirikiana na Serikali kupitia wizara ya Afya katika kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali hususani malaria,kifua kikuu,VVU na ukimwi,huduma bora za maabara na rasilimali watu katika sekta ya Afya.
Kwa upande wake mratibu wa kifua kiku katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema, mwanzoni ilikuwa vigumu kuwatambua watoto wenye ugonjwa huo kwa kuwa walitumia njia ya kuwauliza maswali wazazi,hata hivyo haikuwa njia sahihi ya kubaini vimelea vya kifua kikuu kwa watoto.
Aidha, ameishukuru MDH kutuma wataalam wake  kwenda kufundisha wauguzi na madaktari ambao wamepatiwa uwezo wa kufanya hunguzi wa TB kwa watoto kwa njia ya mpira, mpango ambao utakwenda kumaliza kabisa tatizo  la maradhi  ya ugonjwa huo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano katika wilaya hiyo.
Dkt Kihongole alisema, wahudumu waliopata mafunzo  watapelekwa katika maeneo yote ili kutoa huduma kwa watoto, na litamaliza kasumba ya wazazi na walezi kupeleka watoto kwa Waganga wa Tiba asili na tiba mabadala pindi wanapoona mabadiliko ya afya kwa watoto wao.
Baadhi ya wazazi wamelishukuru shirika hilo kwa kupeleka huduma hiyo ambayo inakwenda kuokoa maisha ya watoto wengi hasa wale wanaopa maradhi ya kifua kikuu.
Wamepongeza mpango huo kwani utawezesha sana kuibua ugonjwa wa TB kwa watoto,kwani kila wanapokwenda Hospitali wakati mwingine wataalam walishindwa kutambua kwa vile walishindwa kupata makohozi kwa ajii ya vipimo.
Rukia Omari na Mwanahawa Musa wa Kijiji cha Misechela wameomba wataalam hao wafike kila kijiji kutoa huduma ya uchunguzi  wa ugonjwa wa kifua kikuu na magonjwa mengine ambayo ni chanzo cha kupoteza maisha ya watoto wengi katika wilaya  ya Tunduru.