Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka Wizara ya Ardhi, Hamdouny Mansour (mwenye sweta
nyeupe) akitoa maelezo kwa wajumbe kuhusu eneo la mpaka linalojulikana kama mafiga matatu
(Tanzania, Ruanda na Burundi) katika bonde la Mto Kagera. Kutoka kulia wa Kwanza ni Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Ulinzi Bwana Ramadhan Kailima akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia
Jenerali Marco Gaguti wa nne (mwenye shati la pinki). Kutoka kushoto ni Nicolous Mkapa, Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Ardhi akifuatiwa na Gerald Mweri, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti (wa pili kutoka kulia) pamoja na wajumbe
waliotembelea mpaka wakimsikiliza mtaalam kutoka Upimaji na Ramani akiwaeleza historia ya eneo la
mafiga matatu (Tanzania, Ruanda na Burundi) katika bonde la Mto Kagera. Nyuma ya Mkuu wa Mkoa ni
alama ya mpaka namba (BP 58), ambayo ndiyo alama ya mwisho ya mpaka kati ya Tanzania na Burundi
kabla ya mto Kagera. Mpaka mwingine mbali na mto kagera ni mto Mwibu ambao unatoa maji nchi ya
Burundi na kuungana na mto Kagera.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Bwana Nicholas Mkapa (aliyevaa miwani) akisikiliza maelezo kutoka
kwa Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Bwana Hamdouny Mansour (wa kwanza kulia)
kuhusu uwekaji wa alama za mpaka katika bonde la mto Kagera ambalo ni mpaka kati ya Tanzania na
nchi za Ruanda na Burundi. Eneo hilo lina historia ya kupakana nchi tatu (Tanzania, Ruanda na Burundi)
na ndiyo maana panaitwa mafiga matatu. Kushoto ni Mthamini Mkuu wa Serikali Bibi Evelyn
Mungashwa na Kulia ni Kamishna wa Ardhi Nchini Bibi Mary Makondo.
Mwenyekiti wa msafara uliotembelea mpaka Dkt. Florens Turuka, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi
akiwasili na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa Wilaya katika Kata ya Bwiigwe Mkoani Kagera kwa
ajili ya ukaguzi wa mpaka eneo la Manyovu.
Dkt. Florens Turuka, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na mwenyekiti wa msafara akijadiliana na
kushauriana na wajumbe wa msafara baada ya kuifikia alama ya mpaka (BP 20) iliyopo eneo la Manyovu
kwenye mpaka wa kuingia na kutoka nchini Burundi. Eneo hili lina historia kwamba ndiyo chanzo cha
mto Malagarasi ambao unatumika kama mpaka kati ya Tanzania na Burundi.
****************************
Na Eliafile Solla
Baadhi ya wananchi wanaoishi katika Kata na Vijiji vya mpakani mwa Tanzania na nchi ya Burundi, wamelalamikia sehemu ya ardhi yao kutumiwa kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu na raia jirani wa Burundi.
Hayo yalijitokeza katika ziara ya Makatibu Wakuu
iliyofanyika katika Mikoa ya Kagera na Kigoma kwa lengo la kukagua maeneo yote ya mpaka wa Kimataifa.
Makatibu Wakuu kutoka Ofisi ya Rais- IKULU, TAMISEMI, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali walifanya ziara Wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, kukagau zoezi la uimarishari wa mpaka uliofanyika mwaka 2014.
Ziara hiyo iliyojumuisha wataalam mbalimbali wanaoshughulikia mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na nchi zinazoizunguka, ilikuwa ya siku nne ambapo wajumbe walitembelea baadhi ya maeneo yaliyopitiwa na zoezi la uimarishaji mpaka lililofanyika mwaka 2014.
Katika ziara hiyo pia, wataalam walitembelea maeneo ya mpaka katika Mkoa wa Kagera ambapo walibaini, baadhi ya raia wa Burundi wanafanya shughuli nyingi za kibinadamu katika maeneo ya mpaka kitu ambacho kiusalama siyo sawa.
Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Florens Turuka ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa wajumbe hao alisema, lengo la kutembelea na kukagua maeneo ya mpaka wa kimataifa uliopitiwa na zoezi la uwekaji wa alama za hifadhi ya mpaka (vigingi) mwaka 2014 ni kukusanya taarifa kutoka kwa wananchi.
Alisisitiza kwamba, taarifa itakayotolewa na wananchi katika maeneo yaliyopitiwa na uimarishaji wa mpaka, itaisaidia Serikali kujua ni mikakati gani iwekwe katika maeneo yanayozunguka mpaka ili kuwalinda wananchi pamoja na mali zao.
Nae mkuu wa Wilaya ya Ngara Luteni Kanali Michael Mtenjele, alisema katika taarifa ya Wilaya kwamba, mpaka kati ya Tanzania na Burundi uko salama na Wilaya imeendelea kuwa na mahusiano na mawasiliano ya karibu na nchi hiyo.
Aliongeza kwamba, mara nyingi zinapotokea changamoto mawasiliano ya simu hufanyika na nchi ya Burundi na kuyatatua kitu ambacho kisingewezekana kama mahusiano yangekuwa siyo mazuri.
Taarifa ya Wilaya pia ilibainisha kwamba, zoezi la uimarishaji mpaka lililofanyika mwaka 2014 liliwaathiri baadhi ya wananchi wa Tanzania waliokuwa wanaishi mpakani.
Kanali Michael alisema, pamoja na athari ambazo tayari Wilaya ilishabainisha, wajumbe wanaweza kupata taarifa zaidi kuhusu hali ya mpaka kutoka kwa wananchi wanaoishi mpakani watakapokuwa wanatembelea na kukagua maeneo hayo.
Pamoja na wajumbe kutembelea na kukagua baadhi ya maeneo yaliyopitiwa na zoezi la uimarishaji mpaka la mwaka 2014, pia walifanya mikutano ya hadhara na wananchi wa
vitongoji na vijiji husika ili kupata taarifa ya hali ya mpaka. Katika mikutano hiyo ya hadhara, baadhi ya wananchi walisema, zoezi la uimarishaji mpaka la mwaka 2014
liliwaathiri wao na mali.
Bibi Jesca Lameck mwenye umri kati ya miaka 75-80 ni mmoja kati ya wananchi waliosema zoezi la uimarishaji wa mpaka la mwaka 2014 lilimuathiri.
Bibi Jesca alisema, katika zoezi hilo lililohusisha uwekaji wa alama (vigingi) katika hifadhi ya mpaka, alijikuta sehemu ya shamba lake la miti, kahawa, matunda na makaburi vikiangukia upande wa nchi ya Burundi.
Baada ya kutembelea na kufanya mikutano na wananchi waliopitiwa na zoezi la uimarishaji mpaka la mwaka 2014, mwenyekiti Dkt Florens Turuka, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi alipokea taarifa kuhusu athari zilizotokana na zoezi hilo, pamoja na changamoto nyingine zinazohusu mpaka tofauti na za uwekaji alama za hifadhi ya mpaka.
Aliushukuru uongozi wa Wilaya ya Ngara kwa jinsi unavyosimamia mahusiano na nchi ya Burundi na kuahidi
kuifikisha mbele zaidi taarifa aliyoipata kuhusu changamoto za mpaka wa Tanzania na Burundi.