Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sita akipokea mashuka na foronya zilizotolewa na vikundi vya ushirika vya Halmashauri hiyo, wanaoshuhudia ni wanakikundi hao pamoja na Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri hiyo Ndugu Salehe Hija .
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sita akikata utepe kwa ajili ya kuzindua mfumo wa usomaji data leo wakati alikuwa akikabidhiwa vifaa vya Hospital na vyama vya ushirika kutoka katika Halmashauri hiyo.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Mhe. Benjamini Sita , akizungumza na vikundi vya ushirika wakati akikabidhiwa vifaa vya Hospital vilivyotolewa na vikundi hivyo. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri hiyo Ndugu Salehe Hija .
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sita akisamiliana na Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri hiyo Salehe Hija.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sita akimkabidhi mashuka Mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kigogo mara baada ya vyama hivyo kumkabidhi vifaa hivyo.
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri hiyo Ndugu Salehe Hija, mwenye miwani akimueleza jambo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sita wakati alipokuwa akipokea magodoro kutoka vikundi vya ushirika.
***************************
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sita amevipongeza vyama vya ushirika vilivyopo katika Halmashauri hiyo kwa kujitolea vifaa vya Hospitali katika Kituo Cha Afya cha Kigogo.
Aidha vyama hivyo vimemkabidhi Mhe. Sita Magodoro 30, mashuka na foronya 150 ambapo wamesema kuwa vitasaidia wagonjwa watakaokuwa wanapatiwa matibabu katika kituo hicho.
Akizungumza na vyama hivyo kabla ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Meya Sita amesema kuwa vitasaidia kuwahudumia wananchi mbalimbali watakao kuwa wanapatiwa huduma katika Kituo hicho cha Afya na kuwasihi wengine kujitokeze kuchangia.
Amefafanua kuwa suala la Afya ni pana na kwamba Halmashauri iliamua kujenga Kituo hicho cha Afya ili kuwezesha wananchi kupata huduma kwa haraka na urahisi kutoka maeneo mbalimbali.
Ameeleza kuwa, Halmashauri ya Kinondoni inahudumia watu kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Bagamoyo, na kwamba kulingana na wingi huo, imeweza kununua eneo hilo na kujenga Kituo hicho cha Afya na kwamba watu kutoka shemu mbalimbali watapata huduma safi na bora inayokidhi viwango.
Ameongeza kuwa” Tumepambana usiku na mchana, na mpongeza sana Mkurugenzi wetu , Ndugu Aron Kagurumjuli na watendaji wote kwa kufanikisha ujenzi wa Kituo hichi cha Afya, ambacho kitahudumia watu sio Kigogo tu , bali kitatoa huduma Ilala, Ubungo, na maeneo mengine kama ilivyo kwa Kituo cha Afya cha Magomeni.” amesema Meya Sita.
Hata hivyo Mhe. Sita emesema “ ninawapongeza sana, ninaimani wadau wengine watakapo ona hivi, itawakumbusha kuona kwamba wanawajibu kufanya hivi kama walivyofanya hawa vyama vya ushirika kutambua umuhimu wa afya katika Halmashauri yetu” ameongeza.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji, na Ushirika , Ndugu. Salehe Hija amekipongeza kitengo cha ushirika kwa kuandaa vifaa hivyo na kukabidhi katika Kituo hicho cha Afya na kusema kuwa kitendo hicho kitaonyesha njia kwa watu wengine kujitolea.
Aidha Hija amesema kuwa vifaa hivyo vilivyotolewa vinathamani ya shilingi milioni 6.7 huku kituo hicho kikiwa na uhitaji wa vitanda 150 ambapo kwa mujibu wa mganga mfawidhi wa Kituo hicho , magodoro hayo yaliyotolewa ni ni sawa na asilimia 20 ya mahitaji hayo.