Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga akiongea katika kongamano la kutathimini na kutafakari jitihada zilizofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika kuwakomboa watanzania kwenye haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni lililofanyika jijini Arusha Desemba 13-14, 2019.
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi za umma na binafsi pamoja taasisi za kimataifa.
Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Godfrey Mulisa akiteta jambo na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga walipokutana katika kongamano hilo.
………………
Na Mbaraka Kambona,
Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga amesema kuwa ili serikali iweze kutimiza haki za msingi za binadamu kwa wananchi wake kikamilifu inahitaji nguvu ya kifedha ili kujenga uchumi imara utakaoweza kutimiza haki hizo.
Balozi Mahiga alitoa kauli hiyo kwenye kongamano la kitaifa la kutathimini hali ya haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni lililofanyika jijini Arusha Desemba 13-14, 2019.
Mahiga alisema katika kongamano hilo kuwa ili serikali iweze kutekeleza na kutimiza haki za binadamu ni lazima ijenge mfumo wa uwajibikaji na uwazi ambao utajenga uchumi imara utakaosaidia kutekeleza haki za msingi za binadamu na utawala bora.
Mahiga alisema kuwa kwa kutambua hilo serikali ya awamu ya tano iliamua kwa dhati kabisa kuimarisha mfumo wa ukusanyaji kodi kwa kuziba mianya yote iliyokuwa inapoteza mapato ili kupata fedha za kutosha kutoa huduma kwa jamii.
“Serikali ya awamu ya tano imeleta sio tu mageuzi bali imeleta mapinduzi, kuna vitu ambavyo vilihitaji ujasiri wa pekee kuvitekeleza, huwezi kujenga uchumi kama huna fedha, bila kodi huwezi”,alisema Mahiga
“Kutimiza haki za binadamu kunahitaji mtaji, lazima ujenge mfumo wa serikali bora, serikali ambayo inajenga uchumi wake kupitia mapato yake ya ndani kama serikali ya awamu hii inavyofanya”,aliongeza
Mahiga aliendelea kusema kuwa serikali imepambana na mianya ya kuvuja kwa mapato na ndio maana leo tunashuhudia haki za kijamii, kiutamaduni na kiuchumi zinatekelezwa kwa vitendo.
Alisema serikali imeendelea kuwapa watu wake fursa mbalimbali za kiuchumi ili kuboresha hali za maisha yao kwa mtu mmoja mmoja hata vikundi.
Mahiga alisema serikali itaendelea kutekeleza mpango wa taifa wa miaka mitano (2016, 17-2020/21) ambao umelenga kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.
Alisema kuwa uamuzi wa serikali wa kujenga uchumi wa viwanda unalenga kuleta maendeleo jumuishi na endelevu kwa kutumia ipasavyo rasilimali zilizopo na hivyo kuchangia katika kukuza pato la taifa na kutoa nafasi nyingi na endelevu za ajira.
Aidha, alisema kuwa katika kutimiza haki ya elimu, serikali imechukua hatua kadhaa ikiwemo utekelezaji wa sera yake ya elimu ya msingi na sekondari bila malipo. Sera hii imesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kutoka milioni 1.57 mwaka 2015 hadi milioni 2.08 mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 35.2.
Kuhusu haki ya afya, Mahiga alisema serikali imeendelea kuimarisha vituo vya afya, imeongeza bajeti ya dawa kutoka bilioni 31 mwaka 2015/16 kufikia bilioni 270 mwaka 2018/19. Ongezeko hilo limeongeza upatikanaji wa dawa muhimu kufikia asilimia 96 kwa mwaka 2018/19. Tiba za kibingwa zinatolewa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, hospitali mpya za rufaa za Benjamini Mkapa na Mloganzila. Hospitali hizo zinatoa huduma za kibingwa zikiwemo upasuaji wa moyo, ubongo na uti wa mgongo ambazo awali zilikuwa zinapatikana nje ya nchi .
Awali , Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni kutathimini na kutafakari jitihada zilizofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika kuwakomboa watanzania kwenye haki za kiuchumi,kijamii na kiutamaduni.