Home Mchanganyiko CHUO CHAMIPANGO CHASHAURIWA KUANZISHA VIWANDA KANDA YA ZIWA

CHUO CHAMIPANGO CHASHAURIWA KUANZISHA VIWANDA KANDA YA ZIWA

0

Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Dkt. Emmanuel Kipole wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa Mahafali ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Kanda ya Ziwa-Mwanza. Kulia kwake ni Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof. Hozen Mayaya na kushoto kwa mkuu wa wilaya ni Kamishna Msaidizi wa Bajeti Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Pius Mponzi.

Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kanda ya Ziwa wakiwa katika sherehe ya Mahafali ya 33 yaliyofanyika kwa mara ya saba katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza.

Kamishna Msaidizi wa Bajeti Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Pius Mponzi akihutubia wahitimu na wageni mbalimbali waliohudhuria katika sherehe za Mahafali ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kanda ya Ziwa, tawi la Mwanza.

Mkuu wa wilaya ya Sengerema Dkt. Emmanuel Kipole ambaye ni Mgeni Rasmi kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, akihutubia wahitimu wakati wa Mahafali ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini cha Kanda ya Ziwa kilichoko Jijini Mwanza

Mkuu wa wilaya ya Sengerema na Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini cha Kanda ya Ziwa, Kituo cha Mwanza yaliyofanyika kwa mara ya saba katika Kituo hicho, Dkt. Emmanuel Kipole,  akimtunuku mmoja wa wahitimu katika sherehe zilizofanyika jijini Mwanza.

Meza Kuu ikiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Sengerema Dkt. Emmanuel Kipole wakiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa kada mbalimbali wakati wa Mahafali ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika kwa mara ya saba katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Mwanza)

……………………

Na Saidina Msangi na Ramadhani Kisimba, WFM, Mwanza

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amekiagiza Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kuanzisha viwanda katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kuchochea maendeleo ya vijana na wananchi kwa ujumla.

Maagizo hayo yametolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Dkt. Emanuel Kipole Dkt. Kipole, aliyemwakilisha kuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 33 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kituo cha Kanda ya Ziwa, kilichoko mkoani Mwanza.

‘’ Nimefurahishwa kwa juhudi za Chuo za kuonesha mfano kwa kuanzisha Kiwanda cha Kukamua Alizeti katika Kijiji cha Pahi, Kata ya Pahi, Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma na ni matumaini yangu kuwa Chuo kitaendelea kukisimamia kwa ufanisi kiwanda hiki ili kiweze kuchochea maendeleo kwa vijana na wananchi wanaozunguka eneo la mradi huo’’ alisema Dkt. Kipole.

Alitoa wito kwa Chuo hicho kuongeza juhudi za kuanzisha viwanda vingine katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa hususani katika Wilaya za Magu na Bariadi ambako Chuo kina viwanja kwa ajili ya  kujenga miundombinu yake ya kudumu’’ aliongeza Dkt. Kipole

Aidha Dkt. Kipole alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani ilidhamiria na imeendelea na dhamira yake ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika taasisi zote za elimu hapa nchini ili kutoa fursa kwa wananchi wengi, hususan wanyonge kupata elimu bora.

“Ili kufikia azma hii, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuondoa ada na michango kwa elimu ya msingi na sekondari na kuongeza ruzuku za kuendeshea shule za msingi na sekondari zote za umma hapa nchini, ambapo kwa sasa Serikali inatoa kiasi cha shilingi bilioni 24 kwa mwezi kwa shule zote za Serikali nchini’ aliongeza Dkt. Kipole

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Idara ya Bajeti ya Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.Pius Mponzi ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu Wizara hiyo, Bw. Doto James, alisema mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yana umuhimu mkubwa kwa nchi hasa ikizingatiwa kwamba watalaamu wa mipango wanahitajika  ili wasaidie kupanga masuala ya maendeleo katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya vijiji hadi Taifa.

Awali Mkuu wa chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Profesa Hozen Mayaya, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais  Dkt. John Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa maelekezo, ushauri na miongozo mbalimbali wanayoitoa kwa Chuo chake ambayo ndiyo imekuwa chachu ya mafanikio ya Chuo hicho.

Profesa Mayaya aliwataka wazazi na walezi kuitumia fursa iliyotolewa na Serikali ya kutoa elimu bure katika ngazi za shule ya msingi na sekondari kuwaandaa vijana ili wapate elimu ya juu itakayowasaidia kuongeza maarifa na kujikwamua katika umasikini