Home Mchanganyiko TBS: VIWANGO 1,587 VIPO TAYARI KULINDA AFYA YA WATANZANIA

TBS: VIWANGO 1,587 VIPO TAYARI KULINDA AFYA YA WATANZANIA

0

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Athman
Ngenya akifafanua kitu kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani), kuhusu
mafanikio ya Shirika hilo katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano,
Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dar es
Salaam leo Desemba 11, 2019.

Picha na Idara ya Habari-MAELEZO

*********************************

Na. Paschal Dotto-MAELEZO 11.12.2019

Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano Shirika la Viwango
Tanzania (TBS) limefanikiwa kutekeleza mambo mbalimbali ili kuwezesha uwepo wa bidhaa safi zenye hadhi kwa matumizi ya wananchi.

 

Katika mkutano wake na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika sla Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Athuman Ngenya amesema kuwa wamefanikiwa kutekeleza azma ya kulinda afya za wananchi kwani mpaka sasa Shirika hilo limeweza kutayarisha viwango 1,587 katika sekta mbalimbali.

 

“TBS kwa kipindi hiki cha miaka minne ya Serikali ya Rais John Pombe Magufuli
tumefanikiwa kutayarisha viwango 1,587 katika sekta za chakula, kemikali,
mazingira, sekta mtambuka, ngozi na nguo, uhandisi (umeme, mitambo, ujenzi, na madini), kwa hiyo viwango hivi vimesaidia wazalishaji na wafanyabiashara
kuzalisha bidhaa zilizo na ubora”, Dkt. Ngenya.

 

TBS wamatekeleza majukumu ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata bidhaa
ambazo ziko safi na zina ubora kwa matumizi ya afya ya binadamu na katika
kutimiza azma hiyo jumla ya sampuli 71,863 zilipimwa katika maabara za TBS
ambayo ni sawa na asilimia 85.6 ya lengo la kupima sampuli 84,000.

 

Aidha Dkt.Ngenya alisema kuwa katika maabara za shirika hilo jumla ya mitambo 21,726 ilifanyiwa ugezi sawa na asilimia 82.5 ya lengo la kufanya ugezi mashine 34,000 ambapo suala hilo limefanyika katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano.

 

Dkt. Ngenya alisema kuwa katika miaka minne ya Rais Magufuli, TBS imeweza
kutoa vyeti vya ubora kwa bidhaa mbalimbali ambazo zimekubalika kulingana na
viwango vya shirika hilo, jumla ya vyeti 1, 137 sawa na asilimia 80.6 vilitolewa kwa bidhaa mbalimbali, na pia hii ilichangiwa na ari ya shirika hilo kusogeza huduma kwa wananchi.

 

Pia katika kipindi hiki cha miaka minne ya Rais John Pombe Magufuli TBS
imefanikiwa kutoa gawio kulingana na Sheria ya Bajeti ya kuwasilisha Serikalini
asilimia 15 ya mapato ghafi na kuchangia pato la Serikali kuanzia mwaka
2016/2017 mpaka Septemba 2019 jumla ya TZS bilioni 34.8 ziliwasilishwa
Serikalini. Katika kuimarisha ufanisi wa kazi TBS lina jumla ya Maabara nane ambapo kati ya hizo sita zimehakikiwa na kupewa vyeti vya umahiri na kutambulika kimataifa na hivyo kumuwezesha mfanyabiashara kupata urahisi wa masoko ya kimataifa.

 

“Kati ya kitu ambacho kwa miaka hii minne ya Serikali ya Awamu ya Tano,
maabara sita za TBS zimethibitishwa kimataifa na kuweza kuleta nafuu kubwa kwa wafanyabiashara kimasoko, maabara hizo ni maabara ya ugezi, chakula, kemia, umeme, mitambo na maabara ya ujenzi, hizi ni maabara ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara wetu”, Alisema Dkt. Ngenya.