Home Mchanganyiko JAMII ISHIRIKIANE NA WAWEKEZAJI ILI KUINUA MAENDELEO NA UCHUMI WA ENEO HUSIKA

JAMII ISHIRIKIANE NA WAWEKEZAJI ILI KUINUA MAENDELEO NA UCHUMI WA ENEO HUSIKA

0
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo ameitaka jamii kushirikiana na wawekezaji katika maeneo yao pamoja na kuwageukia wawekezaji kushiriki kuchangia shughuli za kijamii kwenye maeneo hayo,ili kujiletea maendeleo na kujiinua kiuchumi.
Aidha ametaja ,changamoto ambazo bado zinakabili baadhi ya maeneo ya uwekezaji ni kutokuwa na umeme wa uhakika ,miundombinu ya maji, umeme ,barabara,malighafi pamoja na ukosefu wa masoko.
Aliyasema hayo ,katika mkutano wa mashauriano kati ya serikali wawekezaji na wafanyabiashara wa mkoa huo ,ambapo Mawaziri na Manaibu Waziri wa wizara mbalimbali walifika mji wa Kibaha kutoa ufafanuzi mbalimbali na kuulizwa maswali na wawekezaji na wafanyabiashara hao.
Ndikilo alieleza ,jamii na wawekezaji wanategemeana hivyo hakuna budi kujenga ushirikiano ili kujiletea maendeleo.
Hata hivyo, alifafanua kati ya changamoto za uwekezaji pia lipo tatizo la ucheleweshaji upatikanaji wa vibali,masharti magumu,vibali vya ujenzi na riba kwa taasisi za fedha.
“Baadhi ya maeneo kutotengwa kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo,kupata leseni ya EPZA kwa wawekezaji na kukosa kibali cha chassis ya gari ili kuunganisha bodi za magari,” alisisitiza Ndikilo.
Nae mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Abdala Ndauka alitaja,changamoto mojawapo ni baadhi ya taasisi za zinazohusika na vibali kutumia nguvu badala ya kutoa elimu.
Kwa upande wake mfanyabiashara na mwekezaji wa masuala ya elimu na hotel ya Njuweni,alhaj Yusuph Mfinanga alisema ifikie hatua jamii ikaona thamani ya wawekezaji kwenye maeneo yanayowazunguka na kushirikiana nao pasipo kuwawekea vikwazo.
Alichukua fursa hiyo, kutoa dukuduku lake kuhusiana na hasara aliyoipata baada ya kununua shule ya Mangiyo iliyopo wilaya ya Mwanga,mkoa wa Kilimanjaro,shule kupitia Jumuiya ya Wazazi kihalali ,lakini lilitokea kundi la watu wa kijiji na kudai shule hiyo haijauzwa.
“Nimekwama ,licha ya kununua kihalali, shule hiyo iliyo chini ya Jumuiya ya wazazi miaka minne sasa, lakini uwekezaji wangu umepotea kwakuwa sijanufaika nao, ninaumia,nateseka,naomba Waziri husika na Chama kinisaidie kupata haki yangu”alieleza Mfinanga.
Mfinanga anakiomba chama cha mapinduzi (CCM) kumsaidia kurudishiwa fedha zake ama kuachiwa shule ambayo kainunua ili kuondokana na hasara anayoipata.
Angela Kairuki Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) na baadhi ya mawaziri walitoa majibu kutegemeana na wizara ambapo Kairuki ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti mkutano huo alisema kuwa wanakutana na wadau hao ili kujua changamoto zinazowakabili kwani baadaye wataandaa mipango na mikakati kwa ajili ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Waziri wa ardhi ,William Lukuvi alisema ,amebeba baadhi ya changamoto zilizogusa wizara yake kwani nyingine zinashughulikiwa na zipo katika ufuatiliaji.
Hata hivyo, alibainisha kati ya vijiji ambavyo vilikuwa sehemu ya hifadhi na mheshimiwa Rais kusema maeneo hayo yatakuwa ya makazi mkoa wa Pwani ni vijiji 86 ambapo kwa sasa wanajiandaa kuyapima maeneo hayo na kuyaweka kimipangomiji.
Nae waziri Hasunga alifafanua, wanahimiza uwekezaji kwenye uzalishaji chakula na kwenye pembejeo ikiwemo mbolea ambapo mahitaji ni 186,000 lakini uwezo wa ndani haizidi tani 50,000.
Naye naibu Waziri Mavunde alisema kuwa kwa sasa wanaangalia namna ya kumkopesha kijana mmoja mmoja kwa baadhi ya maeneo kwani baadhi ya maeneo mikopo ya vikundi ni changamoto na utafiti umeonyesha kwa vikundi kuna ugumu.