Home Michezo MO DEWJI  AWASHUKIA MASTAA ATAJA BAJETI YA MAMILIONI

MO DEWJI  AWASHUKIA MASTAA ATAJA BAJETI YA MAMILIONI

0

Na Mwandishi Wetu, 
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Mohammed ‘Mo’ Dewji amesema haridhishwi kabisa na nidhamu ya baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo nje ya uwanja na kwamba bodi anayoiongoza haitavumilia mchezaji yeyote asiyejua thamani ya klabu, kwani kuonyana sasa imetosha.
Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa klabu leo Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, Dewji amesema kwamba amekuwa mnyonge kuona uwekezaji waliouweka kwao, baadhi yao, huutumia kama fimbo ya kuwachapia.
“Niwaambie wachezaji wote, Simba ni klabu kubwa kweli kweli, tena kubwa hasa, na hakuna shaka ni namba moja Afrika Mashariki, bodi ninayoiongoza mimi haitavumilia mchezaji yoyote asiyejua thamani ya Simba. Kuonyana onyana sasa imetosha,” amesema Mo Dewji.

Mohammed ‘Mo’ Dewji haridhishwi kabisa na nidhamu ya baadhi ya wachezaji wa Simba nje ya Uwanja 

Wajumbe wa Bodi katika Mkutano Mkuu wa klabu leo Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam

Wanachama wa Simba katika Mkutano Mkuu wa klabu leo Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere  

“Sisi tunawalipa vizuri mno, na wao wana wajibu wa kutulipa matokeo na furaha. Na ili furaha iwepo, lazima nidhamu isimamiwe kikamilifu, na katika hili hatutanii. Hatutajali ukubwa wa jina la mchezaji yoyote,” ameongeza Mo Dewji.
“Nidhamu kwetu ni muhimu kama tunataka tufikie malengo tuliyokusudia. Na haya ndio yaliyotufanya bodi tuchukue maamuzi magumu kwa kocha wetu. Timu imeshindwa kufikia malengo, kisha nidhamu hakuna, alafu tuvumilie?,” amesema Mo Dewji.
“Simba lazima tuamue kuteseka na moja katika mambo haya mawili, (1) tuzoee uchungu na maumivu ya nidhamu au (2) maumivu ya matokeo mabaya. Kama mpenzi wa Simba, siwezi. Mtaniwia radhi kidogo, nimekuwa mkali ila nidhamu kwangu ndio kila kitu. Hata mimi mwenyewe naishi kwa nidhamu, na ndio siri ya mafanikio yangu,” amesema Mo Dewji. 
“Klabu yetu imeimarisha sana timu zake za vijana na wanawake, na sasa sisi ni miongoni mwa klabu chache Tanzania zenye timu imara za vijana chini ya miaka 20, na ile ya miaka 17, na tuna timu nzuri ya wanawake, na tunazidi kuziimarisha,” ameongeza Mo Dewji.. 
“Na katika msimu huu wa ligi, tutahakikisha tunachukua tena ubingwa ili tuje kuweka rekodi nyingine kwenye klabu bigwa Afrika. Nawahakikishia wanachama wenzangu kujikwaa si kuanguka, hatutarudia makosa! Insha’Allah, Mungu atutangulie,” ameongeza Mo Dewji.. 
aidha, Mo Dewji amesema kwamba wana mpango wa kufungua akademi ya Simba ili baadaye waje kuvuna vijana vilivyolelewa kwenye mfumo na asili ya klabu hiyo kwa  kuwafundisha vijana hao thamani ya klabu na falsafa ya uchezaji wake pamoja upendo ili wawe na uchungu zaidi na klabu.
“Msimu uliopita ulikuwa mzuri sana kwetu kwa ujumla wake. Kucheza hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na kisha kuvuka hadi robo fainali ilikuwa ni jambo kubwa kwa klabu, ukizingatia pia tuliweza kutetea ubingwa wetu wa nchi,” ameongeza Mo Dewji.
“Kuzifunga nyumbani klabu kubwa kama Mbabane, Nkana, Soura, Ahly na AS Vita ilikuwa ni heshima kubwa. Hususani tulikuwa tukiwafunga mbele ya mashabiki wetu 60,000 waliokuwa wakituunga mkono kwa hali na mali. Binafsi msimu uliopita ulikuwa amazing,” ameongeza Mo Dewji.