Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi Haroun Ali Suleiman akitoa ufafanuzi kwa Vikundi vya Ujasiriamali vya kuweka na kukopa vya shehia ya Ng’anani na Kajegwa Makunduchi kuhusu kuvisaidia zaidi Vikundi hivyo.
Miongoni mwa Wanavikundi vya Ujasiriamali vya kuweka na kukopa vya shehia ya Ng’anani na Kajegwa Makunduchi Bimkubwa Bereka akisoma risala ya Vikundi hivyo katika hafla iliyofanyika Skuli ya Msingi Kajegwa Makunduchi.
Baadhi ya Wanavikundi vya Ujasiriamali vya kuweka na kukopa vya shehia ya Ng’anani na Kajegwa Makunduchi Wakimsikiliza Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi Haroun Ali Suleiman huko Skuli ya Msingi Kajegwa Makunduchi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud akiwakabidhi pesa Baadhi ya Wanavikundi vya Ujasiriamali vya kuweka na kukopa kutoka shehia ya Ng’anani na Kajegwa Makunduchi katika hafla iliyofanyika Skuli ya Msingi Kajegwa Makunduchi.
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
……………………
Na Mwashungi Tahir
MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja Ayoub Mohamed Mahmoud amevitaka vikundi vya wajasiriamali vya kuweka na kukopa shehia ya Ng’anani na Kajengwa Makunduchi kuwa na mashirikiano ili kufanya kazi zao kwa vizuri.
Aliyasema hayo huko Skuli ya Msingi Kajegwa Makunduchi Wilaya ya Kusini wakati wa kutambulishwa kwenye vikundi hivyo vya Ujasiriamali vya kuweka na kukopa na kuwataka kuendelea kufanya kazi zao kwa kuwa na mashirikiano ili kupata ufanisi zaidi.
Amesema iwapo watakuwa na mashirikiano katika utendaji wao wa kazi kutaweza kuwapatia fursa za kuongeza kipato chao na kujikwamua kimaisha pia kuacha kuwa tegemezi kwani akinamama ndio wenye mipango mingi ya maendeleo.
Aidha amesema wajasiriamali wana uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yao kwa kazi zao wanazozifanya hadi kujikuta wanakuwa matajiri , kwani matajiri wote wameanza biashara ndogo ndogo mpaka wamefika katika hali nzuri.
“Wengi walikuwa kipato chao cha chini na wameanza kufanya biashara ndogo ndogo hadi sas wamekuwa matajiri wakubwa hivyo msivunjike moyo”, aliwaasa Mkuu wa Mkoa huyo wa Kusini.
Pia amesema Serikali imeweka Sera katika Ilani ya Utekelezaji wa CCM kwa vikundi vya ujasiriamali na kupatiwa mikopo ya kuweka na kukopa kwa lengo la kujiletea maendeleo.
Ayoub ameahidi kuvisaidia vikundi hivyo vya wajasiriamali vya kuweka na kukopa kama vile mabusati, kuwandalia mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kufanya shughuli zao zaidi na kuwa na taaluma nzuri na kuwahimiza wajitahidi kurudisha mikopo kwa haraka ili mitaji iweze kukua kwa vizuri.
“Nawaombeni sana mujitahidi kurejesha mikopo kwa wakati ili matarajio yenu yaweze kufikia katika kujikwamua kimaisha”, alisema Ayoub.
Jumla ya vikundi hivyo ni 5 ambavyo amewapa sh laki tano kwa kila kikundi ambapo vikundi hivyo ni Kubihi moyo, Tuwe wakweli , Fikira zetu , Anacho hapokonyeki na Tuaminiane kwa lengo la kuendeleza kazi zao.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi Haroun Ali Suleiman amesema vikundi hivyo vya akinamama viko katika hali nzuri na kuvitaka vizidi kuimarika ili viwe mifano kwa vikundi vyengine.
Amesema atazidi kuvisaidia ili vizidi kuwa imara na kuwataka wawe mstari wa mbele kutoa taaluma waliyonayo kwa wale wanaotaka kupotea katika maadili yao ndani ya Mkoa huo.
Amewataka wazidi kuendelea kupendana na kila kikundi amewazawadia sh Laki tano kwa kila kikundi kwa lengo kujiimarisha zaidi.
Kwa upande wa msoma risala wa vikundi hivyo Bimkubwa Bereka Mbaraka alisema kila kikundi kina wanachama 30 na wanafarijika kwa kupata muongozo mzuri kwa Mwakilishi wao na kumshukuru kuwa muadilifu kwao.
Alisema kwa upande wa mafanikio wameweza kuunganika na kuwa kitu kimoja katika harakati zote za kijamii.
Pia alielezea changamoto zao zinazowakabili ni pamoja na wanachama kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati , kuwa na uhaba wa elimu ya ujasiriamali na kuendeha vikundi na uwekaji wa kumbukumbu kwa mfumo wa kitaaluma.