Happy Lazaro,Arusha
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini wanapaswa kuleta Mabadiliko chanja katika jamii inayowazunguka na kuweza kuchochea maendeleo ambayo yataleta tija na sio vinginevyo.
Ameyasema hayo Jana wakati akiwatunuku wahitimu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru(TICD) wilayani Arumeru katika ngazi ya Astashahada,Stashahada na Shahada katika maendeleo ya jamii katika mahafali ya tisa akiwataka kuwa chachu ya kuleta mabadiliko katika jamii inayowazunguka.
Waziri huyo amesema kutokana na maarifa wanayokua wamepata katika nyanja mbalimbali wanapaswa kutumika kikamilifu kwa halmashauri kuwatengea bajeti kama zinavyofanya kwa kada zingine badala ya kuwatumia kwa dharura wakati wamepewa mbinu za kuhamasisha maendeleo.
Ametoa wito kwa wahitimu kuacha kulalamika juu ya ajira bali wawe wazalendo kwa kuanza kujitolea katika kazi na kuzingatia maadili ya taaluma yao kwa kuzingatia mazingira ya maeneo watakayokua wanafanya kazi.
Pia ameitaka taasisi hiyo kuwa wabunifu katika kubuni vyanzo vya mapato zaidi vya kuiwezesha kutatua changamoto za kifedha zinazowakabili wakati serikali ikiendelea kuahidi kutekeleza wajibu wake kwa taasisi hiyo.
Ameagiza Bodi ya uongozi kupitia mtaala wa taasisi hiyo kuona kama unaenda na wakati kwa kumwezesha mhitimu kuajirika na kujiajiri mwenyewe baada ya uzoefu kutoka kwa waajiri kuonesha wahitimu wengi wanakosa stadi za kazi.
Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dk John Jingu ametoa wito kwa wahitimu kuitumia elimu waliyoipata kufungua fursa mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za kimaisha na kuwa kielelezo kwa mwenendo mwema katika jamii inayowazunguka.
Amesema kuwa kada ya Maendeleo ya Jamii ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote duniani na serikali inathamini mchango unaotolewa na wataalamu hao kwani imekuwa msaada mkubwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
Naye Mkuu wa taasisi hiyo,Dk Bakari George amesema kuwa wahitimu wamepewa stadi sahihi na kutoa rai ya kwenda kuleta mabadiliko katika jamii kwa kuhakikisha wanakuwa chachu ya mabadiliko na kutengeneza fursa za ajira kwa wengine.
Aidha jumla ya wahitimu 918 wametunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali katika fani za Maendeleo ya Jamii, upangaji wa miradi na jinsia.