Katibu Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Omar Hassan King akizungumza na Viongozi wa Wasanii wa Maigizo kutoka Wilaya zote za Unguja, Kikao kilichofanyika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Mjini Zanzuibar.
Mjumbe wa Bodi ya Wasanii Zanzibar Mussa Makame Pandu akitoa maelezo kwa Viongozi wa Wasanii (hawapo Pichani) katika kikao kilichofanyika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo.
Na Kijakazi Abdalla – Maelezo 7/12/2019
WASANII wa Sanaa za maigizo Zanzibar wametakiwa kuzisajili kazi zao katika Ofisi ya Msajili wa Hakimiliki Zanzibar (COSOZA) ili kuzilinda na kupata haki stahiki zao.
Akizungumza katika kikao cha Viongozi wa Wasanii wa maigizo Katibu Mkuu Wizara ya Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Omar Hassan (Kingi) huko katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo Zanzibar.
Amesema iwapo wasanii kazi zao hawatozisajili katika taasisi hiyo itakuwa vigumu kwa taasisi kuwa na nguvu ya kuweza kuzitetea kazi zao na kupata haki stahiki.
Amesema kumekuwepo na malalamiko ya wasanii kukosa haki zao hii inatokana wasanii kutojisajili katika ofisi hizo na kushindwa kuzitambua kazi zao
Aidha Katibu Kingi amesema kuwa Sanaa ya maigizo Zanzibar imeshuka hivyo ipo haja ya kuchukuwa juhudi ya kuhakikisha Sanaa hiyo inakuwa kwa kasi kubwa na kuweza kulinda maslahi yao.
Amesema kuwa katika kuitambua suala hilo Wizara imeweza kuchukua hatua ya kuratibu wasanii kila wilaya ili kuwatambua umuhimu wao katika kazi zao pamoja na kuwaengezea kipato.
Vilevile amesema kuwa ipo haja wasanii wa Zanzibar kuzirejesha Sanaa za maigizo ya kizamani ili kuweza kulinda mila silka na utamaduni wa visiwa hivi jambo ambalo linaonekana kutoweka.
Hata hivyo amewataka wasanii wa Zanzibar kuwa na umoja wa wasanii ili kuwatambua wasanii wa zamani na wapya ambao wanachipukia katika kazi hiyo.
Amesema kuwa hivi sasa wasanii wa Zanzibar wamekuwa hawana umoja jambo ambalo limekuwa vigumu kuweza kuwasaidia pale inapotokea wanahitaji misaada ya kiserikali.
Aidha amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wasanii wa Zanzibar wanafaidika na kazi zao kwa kuutambua mchango wao waliotoa katika kazi ya tasnia hiyo.