Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiangalia ujazo wa maji kwenye tenki la Mradi wa Maji wa Busisi, wilayani Sengerema.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwa kwenye Mradi wa Maji wa Nyampande katika Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza ambao ujenzi wake umefikia asilimia 40.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akipokea maelezo kuhusu Mradi wa Maji wa Nyamazugo unaohudumia mji wa Sengerema kutoka kwa Naibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akitoa maelekezo kwa wataalam mara baada ya kukagua Mradi wa Maji wa Nyakalilo-Bukokwa katika Halmashauri ya Buchosa, mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Dkt. Charles Tizeba (kulia) mara baada ya kukagua Mradi wa Maji wa Nyehunge katika Halmashauri ya Buchosa, mkoani Mwanza.
………………..
Wizara ya Maji imetangaza itatoa vibali kwa ajili ya kuanza kazi ya utekelezaji wa miradi ya maji ya Sima na Nyasigu-Lubingo-Ngoma katika Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametoa kauli hiyo akiwa ziarani katika Wilaya ya Sengerema akikagua miradi ya maji na kukuta kazi ya ujenzi wa miradi hiyo haijaanza kutokana na kukosekana kwa vibali.
Akawatoa hofu wakazi wa vijiji vya Sima, Nyasigu, Lubingo na Ngoma kuwa Serikali imeshatenga fedha za ujenzi wa miradi hiyo na kumuelekeza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga kukamilisha taratibu zote za upatikanaji wa vibali hivyo ili kazi hiyo ianze haraka.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Aweso amewataka Wakala wa Usambazaji wa Maji Vijijini (RUWASA) kuukamilisha Mradi wa Maji wa Nyakalilo-Bukokwa katika Halmashauri ya Buchosa ambao una miaka mitano tangu utekelezaji wake uanze na haujakamilika.
Aweso amesema haiwezekani mradi wa zaidi ya bilioni 1.3 uchukue miaka mitano bila kukamilika na kutochukua hatua zozote, hakuna haja ya kumsubiri mkandarasi na kuielekeza RUWASA kuukamilisha mradi huo haraka.
Aidha, Kaimu Meneja wa RUWASA mkoa wa Mwanza, Mhandisi Warioba Sanya amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi iliyorithiwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema watajipanga kukamilisha mradi huo kwa kuwa Shilingi milioni 69 zilizobaki zinatosha kumaliza kazi.