MWENYEKITI wa Baraza la Wazee la Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Ndugu Khadija Jabir, na Vyombo vya Habari juu ya taarifa za uchochezi wa kisiasa dhidi ya CCM zilizotolewa hivi karibuni na Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Seif Sharif Hamad.
**********************************
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
BARAZA la Wazee la Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar limelaani vikali taarifa za uchochezi wa kisiasa dhidi ya CCM, zilizotolewa hivi karibuni na Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Seif Sharif Hamad na kueleza kuwa mwanasiasa huyo ana lengo la kuingiza nchi katika machafuko ya kisiasa.
Kauli hiyo imetolewa jana Mwenyekiti wa Baraza hilo,Khadija Jabir Mohamed wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisi kuu ya CCM kisiwandui ambapo alisema mwanasiasa huyo ameanza kupotosha umma kuhusu mgogoro wao dhidi ya CUF na kuingiza CCM.
Alisema kauli zilizotolewa na mwanasiasa huyo ni za uchochezi na kwamba analeta fitina ndani ya Zanzibar lakini wazee wa CCM wanampa onyo kali kuhusu maneno anayoyatoa.
“Baraza la wazee linakemea kauli zake za Seif Sharif Hamad kwa ukali sana tunamuonya kutokana na kuwa yeye ni mtoto mdogo na amelelewa na CCM wakati akitoka kusoma chuo kikuu hakachukuliwa hivyo anafanya mambo bila ya kujua anachokifanya,”alisema
Alisema mwanasiasa huyo hajui kuongoza katika siasa kutokana na kuwa anafanya mambo hasiyojua mbele yake na kwamba anachokifanya ni kuleta mtafaruku ndani ya Zanzibar.
“CCM ina wazee si chama ambacho kama vingine ambavyo havina wazee wakuweza kukemea mambo ambayo hayakwendi vizuri hivyo kwa niaba ya Baraza la Wazee tutaendelea kumkemea dhidi ya kauli zake za uchochezi,”alisema Mwenyekiti huyo.
Naye Katibu Msaadizi wa Baraza hilo la Wazee Haji Machano Haji alisema hivi karibuni mwanasiasa huyo alisikika akiwasingizia vijana wa CCM kuwa wanandoa bendera za chama cha ACT Wazalendo kwenye matawi jambo ambalo ni la uzushi na kwamba ugombi wa majengo ya matawi kati ya vyama hivyo unawahusu wao wenyewe.
Katika maelezo yake alisema Baraza la wazee linampa tahadhari Seif Sharif kuwa anapokaa na wafuasi wake asitoe maneno ya uzushi ama ya fitina hivyo wazee wanamuona mwanasiasa huyo anapaswa kupumzika ili kulinda heshima yake.
“Sisi wazee tumesikia maelezo ya Seif Sharif Hamad aliyoyatoa kwa waandishi wa habari Desemba 2 mwaka huu kwa kukisingizia CCM kwamba inapanga njama ya kuwakamata viongozi wa ACT Wazalendo na kuwambambikizia kesi tunachosema ni mawazo yake,”alisema
Aliongeza kuwa Baraza la Wazee linamuhakikishia Seif Sharif Hamad kuwa CCM haia mkono wowote ndani ya CUF na kwamba wazee wanakitambua chama hicho ni chama cha upinzani kama ilivyo vyama vyengine vya upinzani na mapambano ya chama ni kuvishinda vyama vya upinzani.
Desemba 2 mwaka huu Seif Sharif Hamad alizungumza na waandishi wa habari ofisi ya chama chake cha ACT-Wazalendo ambapo alitoa kauli za uchochezi kwa kuwahamasisha wafuasi wake watumie silaha za jadi kwa ajili ya kuzilinda ofisi za chama chake dhidi ya chama cha CUF ambacho wapo katika mgogoro wa umiliki wa majengo ya ofisi za vyama hivyo.
Seif Sharif Hamad aliwataka viongozi na wanachama wa ngazi zote za chama chake kwa maeneo ya mijini na vijijini kwa upande wa Unguja,Pemba kuzilinda ofisi zote za chama chao na kutoruhusu kuchukuliwa kwa ofisi hizo.
Katika mkutano huo Seif Sharif Hamad alisema wamevumilia vya kutosha na kwamba sasa kutokana na kuwa ni muda mrefu wamevumilia kutokana na maslahi ya nchi lakini wameona wenzeao hawako tayari kuilinda amani.
Maalim Seif alisema wako tayari kumwaga mboga wenzao wakimwaga mchuzi na kwamba alisema chama cha CUF kwa upande wa Pemba kimeanza kuvamia ofisi za ACT-Wazalendo kwa lengo la kuzichukua na kuzifanya ofisi za chama chao kwa madai ni ofisi zao.