Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
(wa pili kutoka kulia) akifuatilia majadiliano katika Mkutano wa Mashauriano kati ya Serikali, Wawekezaji na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Morogoro. Kikao hicho
kimelenga kutatua changamoto katika sekta ya uwekezaji takribani Mawaziri na
Manaibu Waziri 13 wanashiriki kikao hiki.
Baadhi ya Manaibu Waziri Mhe. Ashatu Kijaji na Mhe. Mussa Sima wakiwasikiliza
wachangiaji mbalimbali walioalikwa katika mkutano uliolenga kusikiliza changamoto za Wafanyabiashra uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Glonency mkoani Morogoro.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
akitoa ufafanuzi wa hoja zilizojitokeza katika Mkutano wa Mashauriano baina ya
Serikali, Wafanyabiashra na Wawekezaji katika ukumbi wa Hoteli ya Glonency
mkoani Morogoro.
*******************************
Na Lulu Mussa
Morogoro
Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima amesema Serikali imefanya mapitio ya Kanuni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira ili kurahisha uwekezaji nchi.
Akizungumza na Wafanyabiashara na Wawekezaji katika Mkutano wa Mashauriano baina yao na Serikali katika ukumbi wa Hoteli ya Glonency mkoani Morogoro, Naibu Waziri Sima amesema gharama za kulipia vibali zimepungua na idadi ya siku pia imepungua kutoka siku 145 mpaka siku 95 hivi sasa.
“Ndugu zangu marekebisho haya yote yanayofanywa na Serikali, yanalenga kurahisisha mchakato wa tathmini ya Athari kwa Mazingira na kurahisisha uwekezaji hapa nchini, Mfano awali gharama kwa vituo vya mafuta zilikuwa zaidi ya Milioni kumi na kwa sasa gharama hizi zimepungua hadi kufikia Milioni Nne na nyingine Milioni mbili” Sima alisisitiza.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Sima, amesema Ofisi yake inaandaa Kanuni za Wataalamu Elekezi wa Mazingira ili kurahisisha uwekezaji kwa kuwa miradi yote ni lazima ipate cheti kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). “Tangu tumefanya mapitio ya Kanuni zetu, malalamiko kutoka kwa wawekezaji yamepungua kwa kiasi kikubwa sana” Sima alisisitiza.
Hata hivyo Naibu Waziri Sima amewakumbusha washiriki wa Kikao hicho kuwa Mabadiliko ya tabianchi ni tatizo kubwa duniani, na kutoa rai kwa umma wa watanzania kupanda miti kwa wingi kupunguza athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Amewaagiza wawekezaji hasa wenye Viwanda kuhakikisha wanaanzisha vitalu vya miche katika maeneo yao na kusisitiza kuwa ukaguzi wa masuala ya Mazingira katika maeneo yao utaanzia hapo.
Mkutano huu wa Mashauriano baina ya Serikali, Wafanyabiashara na Wawekezaji
umelenga kusikiliza na kutatua changamoto zao umefanyika leo katika ukumbi wa Hoteli ya Glonency mkoani Morogoro na kuendelea katika Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam. Jumla ya Mawaziri na Manaibu Waziri 13 wanashiriki Mkutano huu.s